Kampuni ya Nike yawasilisha kesi kwa madai ya kuhusishwa na 'Viatu vya shetani'

Muhtasari
  • Kampuni ya Nike inashitaki ubunifu wa kampuni ya MSCHF iliyopo Brooklyn juu ya uzinduzi wa kile kinachosemekana kuwa "Kiatu cha shetani" chenye tone la damu 
  • Kampuni ya MSCHF ilitoa jozi ya viatu 666 Jumatatu ikishirikiana na mwanamuziki Lil Nas X na kusema kwamba vyote viliuzwa chini ya dakika moja
  • Kampuni ya Nike imedai kuingiliwa kwa chapa au alama ya biashara ya kampuni yake

Kampuni ya Nike inashitaki ubunifu wa kampuni ya MSCHF iliyopo Brooklyn juu ya uzinduzi wa kile kinachosemekana kuwa "Kiatu cha shetani" chenye tone la damu ya kweli ya binadamu kwenye soli za viatu.

Viatu hivyo vinavyouzwa kwa dola 1,018 sawa na (pauni 740), ambavyo vimechorwa alama ya msalaba iliyopinduliwa na pentagramu (nyota ya ncha tano katika duara) na maneno "Luka 10:18", vimetengenezwa kwa kuboresha muundo wa kiatu cha Nike Air Max 97s.

Kampuni ya MSCHF ilitoa jozi ya viatu 666 Jumatatu ikishirikiana na mwanamuziki Lil Nas X na kusema kwamba vyote viliuzwa chini ya dakika moja.

 

Kampuni ya Nike imedai kuingiliwa kwa chapa au alama ya biashara ya kampuni yake.

iatu vya rangi nyeusi na nyekundu "vilivyotolewa" na kampuni ya MSCHF Jumatatu, kulikwenda sambamba na uzinduzi wa nyimbo mpya ya mwanamuzi Lil Nas X ya Montero ya (Call Me By Your Name), ambayo ilitolewa kwa mara ya kwanza kwenye mtandao wa YouTube Ijumaa iliyopita.

Katika video ya muziki huo, mwanamuziki huyo wa rapa anateleza kwenye mlingoti kutoka peponi au mbinguni hadi jehanamu au motoni, akiwa amevaa viatu hivyo.

Taswira na hiyo na viatu ambavyo vimeandikwa andiko la Bibilia Luka 10:18 - "Akawaambia, 'Nilimuona shetani akianguka kama radi kutoka mbinguni'."

Kila kiatu kina soli maalum ya muundo wa kampuni ya Nike yenye sentimita za ujazo 60 za wino mwekundu na tone la damu ya binadamu, ambayo ilichangiwa na wanachama wa kampuni hiyo.

Kampuni ya Nike ambayo ni maarufu kwa viatu vya michezo imesema kuwa katika kesi yake iliyowasilishwa kwenye mahakama moja mjini New York, kuwa haiidhinishi au kuruhusu utengenezaji wa 'Viatu vya Shetani'.

Kampuni ya Nike inataka mahakama kusitisha kampuni ya MSCHF kuuza viatu hivyo na pia kuwazuia kutumia nembo yao ya muda mrefu maarufu kama 'Swoosh'.

 

"Kampuni ya MSCHF na viatu vyake vya shetani ambavyo havijaidhinishwa kuna uwezekano mkubwa kukasababisha mkanganyiko na dhana fulani na kutengeneza fikra mbaya kati ya bidhaa ya kampuni ya MSCHF na kampuni ya Nike," Kampuni hiyo ya utengenezaji viatu vya michezo imesema katika kesi yake iliyowasilisha.

"Kwanza, tayari kuna ushahidi wa kutosha unaoonesha mkanganyiko na dhana potovu sokoni, ikiwemo simu zinazotaka watu kususia bidhaa za kampuni ya Nike kufuatia uzinduzi wa viatu vya shetani vya kampuni ya MSCHF, ambavyo inaonekana kana kwamba kampuni ya Nike ndiyo ambayo imeidhinisha na kuruhusu utengenezaji wa bidhaa za hiyo."

Kesi iliyowasilishwa inarejelea ujumbe wa mtandao wa Twitter uliotumwa na mshawishi mkubwa wa viatu @Saint Ijumaa iliyopita, ambao ulianza kuarifu wateja wake kuhusu kuzinduliwa kwa viatu hivyo na kuvipa umaarufu zaidi kwa umma wikendi kwenye mtandao wa kijamii na hata vyombo vya habari vya Marekani.

Baadhi ya wenye msimamo mkali akiwemo gavana wa Dakota Kusini Kristi Noem, na wafuasi wengine wa kidini, wameshutumu viatu hivyo vyenye utata na kumkosoa rapa Lil Nas X na kamupuni ya MSCHF kwenye mtandao wa Twitter.

Hata hivyo, Lil Nas X alimjibu gavana huyo pamoja na viongozi wa kidini kwenye mtandao wa Twitter, na Jumatatu katika mtandao huo, kulikuwa na vibonzo vya mzaha kwenye wasifu wake baada ya kampuni ya Nike kusema kwamba imechukua hatua ya kisheria.