Nike yashinda kesi dhidi ya 'Viatu vya shetani' vyenye tone la damu ya binadamu

Muhtasari
  • Nike yashinda kesi dhidi ya 'Viatu vya shetani' vyenye tone la damu ya binadamu
  • MSCHF ilitengeneza viatu hivyo kwa ushirikiano na mwanamuziki Lil Nas X
  • Kampuni ya MSCHF ilisema kuwa ilitengeneza viatu 666 pekee na vyote tayari vishauzwa

Kampuni maarufu kwa viatu vya michezo ya Nike imeshinda keshi dhidi ya kampuni ya MSCHF juu ya 'Viatu vya shetani' vilivyosababisha utata ambavyo zinasemekana kuwa na tone la damu ya binadamu kwenye soli yake.

Viatu hivyo vinavyouzwa kwa dola 1,018 sawa na (pauni 740), ambavyo vimechorwa alama ya msalaba iliyopinduliwa na pentagramu (nyota ya ncha tano katika duara) na maneno "Luka 10:18", vimetengenezwa kwa kuboresha muundo wa kiatu cha Nike Air Max 97s.

MSCHF ilitengeneza viatu hivyo kwa ushirikiano na mwanamuziki Lil Nas X.

Kampuni ya MSCHF ilisema kuwa ilitengeneza viatu 666 pekee na vyote tayari vishauzwa.

Kampuni ya Nike imedai kuwa MSCHF imetumia nembo yake ya kibiashara na kuomba mahakama kusitisha kampuni hiyo kuuza viatu hivyo na pia iizuie kutumia nembo yao ya muda mrefu maarufu kama 'Swoosh'.

"Kampuni ya MSCHF na viatu vyake vya shetani ambavyo havijaidhinishwa kuna uwezekano mkubwa kukasababisha mkanganyiko na dhana fulani na kutengeneza fikra mbaya kati ya bidhaa ya kampuni ya MSCHF na kampuni ya Nike," Kampuni hiyo ya utengenezaji viatu vya michezo imesema.

Akitoa uamuzi unaopendelea kampuni ya Nike, jaji alitoa agizo la kuzuia uuzaji wa viatu hivyo hapo jana Alhamisi.

MSCHF ilizindua viatu vya rangi nyeusi na nyekundu "vilivyotolewa" Jumatatu, ikiwa ni sambamba na uzinduzi wa nyimbo mpya ya mwanamuzi Lil Nas X ya Montero ya (Call Me By Your Name), ambayo ilitolewa kwa mara ya kwanza kwenye mtandao wa YouTube Ijumaa iliyopita.

Katika video ya muziki huo, mwanamuziki huyo wa rapa anateleza kwenye mlingoti kutoka peponi au mbinguni hadi jehanamu au motoni, akiwa amevaa viatu hivyo.

Taswira na hiyo na viatu ambavyo vimeandikwa andiko la Bibilia Luka 10:18 - "Akawaambia, 'Nilimuona shetani akianguka kama radi kutoka mbinguni'."

 
 

Kila kiatu kina soli maalum ya muundo wa kampuni ya Nike yenye sentimita za ujazo 60 za wino mwekundu na tone la damu ya binadamu, ambayo ilichangiwa na wanachama wa kampuni hiyo.

Katika kesi yake, kampuni ya Nike imesema kuwa haikuidhinisha utengezaji wa viatu hivyo vya shetani.

"Tayari kuna ushahidi wa kutosha unaoonesha mkanganyiko na dhana potofu sokoni, ikiwemo wito wa kutaka watu kususia bidhaa za kampuni ya Nike kufuatia uzinduzi wa viatu vya shetani vya kampuni ya MSCHF, ambavyo inaonekana kana kwamba kampuni ya Nike ndiyo ambayo imeidhinisha na kuruhusu utengenezaji wa bidhaa za hiyo," kampuni ya Nike ilisema.