Rais wa Tanzania kuunda kamati ya kutathmini hali ya corona

Muhtasari
  • Rais wa Tanzania kuunda kamati ya wataalamu ya corona
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Image: HABARI MAELEZO TANZANIA

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametangaza kusudio la kuunda kamati ya wataalamu watakaoshauri juu ya mustakabali wa kukabiliana na corona nchini humo.

Rais Samia amesema Tanzania haiwezi kujitenga kama kisiwa katika janga hilo la corona ambalo linaitikisa dunia kwa mwaka mmoja uliopita.

"Suala la Covid 19 nakusudia kuunda kamati ya kitaalamu. Halifai kulinyamazia bila kufanya tafiti ya kitaalamu. Watuambie upeo wa suala hili... Sio ikitajwa Tanzania basi inakuwa deshi, deshi...Hatuwezi kujitenga kama kisiwa," ameeleza rais Samia.

Rais Samia ameyasema hayo hii leo katika Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha Makatibu Wakuu wa Wizara na wakuu wa mashirika.

Kiongozi huyo amesisitiza pia kamati hiyo itashauri cha kufanyika na si kufuata tu kila kilichopo duniani;

"Rais Kikwete alituambia akili za kuambiwa changanya na zako....Tueleweke kama tunakubali ama kukataa Haifai kulinyamazia tu."

Kauli hiyo ya Rais Samia inadokeza uwezekano wa kubadilika kwa sera rasmi ya mapambano dhidi ya corona nchini humo.

Awali, Tanzania ilianza kwa kuchukua tahadhari za kisayansi mara baada ya kuthibitishwa kuingia virusu hivyo nchini humo katikati ya mwezi Machi mwaka jana. Hata hivyo kadri siku zilivyosogea serikali ilionekana kutochukua hatua zaidi ambazo zimekuwa zikipigiwa chapuo na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama kuweka marufuku ya watu kutokutoka nje.

Tanzania pia iliacha kuchapisha takwimu za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huo mwaka mmoja uliopita. Mwezi Juni Mwaka jana aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hayati John Magufuli alitangaza kuwa nchi hiyo "haina tena maambukizo ya corona kutokana na maombi ya wananchi."

Mapema mwaka huu, Magufuli pia alitangaza kutokuwa na imani na chanjo dhidi ya ugonjwa huo na kuwatahadharisha Wizara ya Afya dhidi ya kuzikimbilia, siku chache baadaye Waziri Doroth Gwajima alitangaza kuwa wizara hiyo haitaagiza chanjo hizo.

Tanzania pia imekuwa ikipigia chapuo matumizi ya tiba mbadala pamoja na kuvuta mvuke wa dawa za asili maarufu kama nyungu, japo vyote hivyo havijathibitishwa na WHO.

Mapema mwanzoni mwa mwaka huu kuliibuka hofu ya wimbi la pili la maambukizi hayo na licha ya taasisi kama Kanisa Katoliki jutoa waraka wa tahadhari na kueleza kuwa watumishi 85 wa kanisa hilo kupoteza maisha kwa kipindi cha miezi miwili wakionesha dalili zote za virusi hivyo.