Bunge la Sudan Kusini lavunjwa

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir avunja bunge la nchi hiyo

Bunge la Sudan Kusini lavunjwa

Muhtasari
  • Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amelivunja bunge,hatua inayotoa njia ya uteuzi wa wabunge
  • Wanaharakati na mashirika ya kijamii wanasema hatua hiyo ilipaswa kufanywa muda mrefu uliopita
  • Wengi wa wabunge 550 watatoka kwa chama kinachotawala cha SPLM

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amelivunja bunge,hatua inayotoa njia ya uteuzi wa wabunge kutoka pande kinzani katika nchi iliyokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano.

Wanaharakati na mashirika ya kijamii wanasema hatua hiyo ilipaswa kufanywa muda mrefu uliopita

Mkataba wa amani uliosainiwa miaka mitatu iliyopita uliamua kwamba karibu robo ya wabunge watatoka kwa chama cha hasimu wa zamani wa Bw Kiir, Riek Machar.

Wengi wa wabunge 550 watatoka kwa chama kinachotawala cha SPLM.

Wabunge wa Sudan Kusini hawatachaguliwa lakini badala yake watateuliwa na vyama tofauti vya kisiasa.

Mzozo uliotokea Sudan Kusini mnamo 2013 ulisababisha moja ya mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu barani Afrika - na watu wasiopungua 380,000 waliuawa na mamilioni wakilazimishwa kutoka nyumbani kwao.

Serikali ya umoja imekuwepo kwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini kufuatia kuzuka kwa mzozo wa kikabila Umoja wa Mataifa umetahadharisha juu ya hatari ya kutokea tena kwa mzozo mkubwa nchini Sudan Kusini.

Mhariri wetu wa Afrika anasema bado kuna changamoto kubwa Sudan Kusini ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa jeshi jipya la kitaifa - linaloundwa na wanajeshi kutoka pande zinazopingana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Ripoti ya hivi karibuni ya UN imetaka zuio la silaha kuongezwa, na kwa vikwazo vipya dhidi ya watu ambao wanazuia utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Ukosefu wa usalama bado umeenea kote Sudan Kusini na imezuia wakulima wengi - ambao wamelazimika kukimbia makazi yao - kupanda au kuvuna mazao, na kusababisha uhaba wa chakula nchi nzima.

Kuna maonyo pia kutoka kwa Mpango wa Chakula wa Ulimwenguni wa UN kwamba zaidi ya watu milioni saba nchini Sudan Kusini watapata uhaba mkubwa wa chakula kwa miezi ijayo.