Mto mtakatifu wa India umejaa miili ya waathirika wa corona

Muhtasari
  • Mto mtakatifu wa India, Ganges, siku za hivi karibuni umekuwa na maiti zilizotapakaa kila mahali ambao ni waathirika wa corona

Mto mtakatifu wa India, Ganges, siku za hivi karibuni umekuwa na maiti zilizotapakaa kila mahali ambao ni waathirika wa corona.

Mamia ya maiti zimepatikana zikielea juu ya mto huo au zikiwa zimezikwa kwenye kingo za mto. Wanaoishi karibu na eneo hilo jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh wanahofia kuwa huenda hao ni waathirika wa virusi vya ugongwa wa Covid-19.

India imeathirika kwa kiasi kikubwa na wimbi la pili la virusi vya corona wiki za hivi karibuni. Pia imerekodi zaidi ya maambukizi milioni 25 na vifo 275,000 lakini wataalamu wanasema idadi halisi ya waliofariki dunia ni juu sana kuliko hiyo.

Miili iliyopo kwenye kingo za mto huo ambayo inakusanywa na kufanyiwa sala ya mwisho na kuchomwa moto kama ilivyo katika tamaduni zao, imekuwa mingi kiasi cha nafasi iliyopo kuashiria kutotosha, hali hiyo ikiwa inaleta taswira ya hali halisi, hasa takwimu ambazo huenda hazijatambuliwa rasmi.

Taswira hii ya kutia hofu katika jimbo la Uttar Pradesh ilianza kubainika mara ya kwanza Mei 10, pale maiti 72 zilipoanza kuelea hadi kwenye kingo za mto huo.

Maafisa wamesema baadhi ya mabaki huenda yakawa ni viungo vya mwili vilivyopatikana juu ya mto Ganges baada ya miili kuchomwa moto kando kando ya mto lakini pia polisi inashuku kwamba kuna maiti zilizopelekwa na kuachwa ndani ya mto

Na siku moja baadaye, miili kadhaa ilipatikana ikiwa imeoza kwenye ukingo wa mto kijiji cha Gahmar huku mbwa na kunguru nao wakiwa wamepata mavuno.

Wenyeji walisema kuwa miili hiyo imekuwa ikielea juu ya mto na kwenye kingo kwa siku kadhaa lakini mamlaka ya eneo hilo imekuwa ikipuuza malalamishi yao juu ya harufu mbaya iliyokuwa imetanda kijijini hadi taarifa hizo zilipoanza kugonga vichwa vya habari.

Miili mingine kadhaa iliyokuwa imefura na kuoza pia ilionekana na wenyeji waliokuwa wameenda kwenye mto huo mtakatifu kuomba. Gazeti la Hindustan limeripoti kwamba polisi waliopoa miili 62.

Katika maeneo ya Kannauj, Kanpur, Unnao, na Prayagraj, kingo za mto huo zimezingirwa na makaburi yaliyochimbwa kina kifupi. Video zilizotumwa kwa BBC zinaonesha makaburi kadhaa. Yanaonekana kama tuta la kitu lakini kila tuta lina mwili uliofukiwa. Katika eneo jirani la Mahadevi ghat, takriban miili 50 ilibainika.

'Miili mingi inayoachwa mtoni' inaonesha idadi ya wanaohesabiwa si sahihi

Kiutamaduni, Wahindu huwa wanachoma miili ya walofariki dunia. Lakini jamii nyingi zinafuata kile kinachofahamika kama "Jal Pravah" - utamaduni wa kuacha miili ikiwa inaelea juu yam to hasa ya watoto, wasichana ambao hawajaolewa, au wale waliofariki dunia kutokana na magonjwa ya kuambukiza au kuumwa na nyoka.

Idadi kubwa ya watu ni maskini na hawawezi kumudu gharama za kuchoma mwili na hivyo basi huwa wanaifunga vizuri kwa nguo nyeupe na kuipeleka majini. Wakati mwingine miili hiyo huwa inafungwa kwenye mawe kuhakikisha mabaki yanadidimia.

Kile ambacho sio cha kawaida ni kwamba wanaoachwa mtoni sasa hivi idadi yao ni kubwa mno na katika maeneo mengi kwa wakati mmoja, ikiwa ushahidi tosha kwamba idadi inayotolewa na serikali sio sahihi.

Mwandishi wa BBC amesema watu 196 wametambulika rasmi kuaga dunia kutokana na virusi jimbo la Kanpur kati ya Aprili 16 na Mei 5 lakini data kutoka maeneo sana ya kuchoma miili inaonesha watu 8,000 wamechomwa moto.

"Maeneo yanayochoma miili kwa kutumia umeme sasa hivi yanafanyakazi saa 24 katika mwezi wote wa Aprili. Lakini pia haikutosha na mamlaka iliruhusu utawala kutumia maeneo ya nje kutumiwa katika shughuli ya uchomaji kwa kutumia kuni," alisema.

"Lakini miili pekee inayopokelewa ni ile ambayo imetoka hospitali yenye cheti cha kuthibitisha vifo vimetikana na corona huku idadi kubwa ya watu wakifariki majumbani bila kufanyiwa vipimo. Na familia zao zikaamua kupeleka miili hyo katika maeneo jirani ambako hakukuwa na kuni wala maeneo ya kuchoma miiili na hivyo basi wakaamua kuizika kwenye kingo za mto."

"Inauma moyo sana. "Watu wote hawa walikuwa kijana, binti, kaka, baba na mama ya mtu. Wanastahili kuzikwa kwa heshima lakini hata hawakuwa miongoni mwa waliohesabiwa - wamefariki dunia bila kutambulika na wamezikwa bila kujilikana."

Wanazikwa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tano usiku

Kubainika kwa makaburi na miili iliyooza na hofu ya kupata maambukizi ya virusi vya corona, kulishitua watu wanaoishi katika vijiji vinavyopakana na kingo za mto huo.

Ukiwa chanzo chake ni Himalayan, mto Ganges ni mmoja kati ya mito mikubwa duniani. Wahindu wanauchukulia kuwa mto mtakatifu, wanaamini kuwa kuoga katika mto huo kutatakasa madhambi yao na huwa wanautumia katika desturi zao za kidini.

Katika maeneo ya Kannauj, Jagmohan Tiwari, mwanakijiji mmoja, 63, alikiambia chombo cha habari cha eneo hilo kuwa ameona makaburi "150-200" katika kingo za mto. "Watu wamekuwa wakizikwa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tano usiku," amesema. "Inaumiza moyo sana."