Mji wa Goma wakumbwa na mlipuko wa pili wa volkano

Muhtasari
  • Mji wa Goma wakumbwa na mlipuko wa pili wa volkano
  • Mlipuko wa pili wa volkano umetokea karibu na mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
  • Ujumbe huo umesema lava imetiririka kuelekea sehemu ambayo haina makazi ya watu katika Mbuga ya Virunga

Mlipuko wa pili wa volkano umetokea karibu na mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Wizara ya mawasiliano ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kupitia ujumbe wa Twitter imesema mlipuko huo ulikuwa mdogo na ulitokea upande wa kaskazini mwa Nyamulagira.

Ujumbe huo umesema lava imetiririka kuelekea sehemu ambayo haina makazi ya watu katika Mbuga ya Virunga.

Makumi ya maelfu ya watu wanaendelea kuhama kutoka mji wa Goma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na hofu ya mIlipuko mingine ya volkano.

Mamlaka za eneo hilo zilisema awali kwamba palikuwa na hofu kwamba Mlima Nyiragongo unaweza kulipuka tena.

Wiki jana mlipuko wa volkano katika mlima wa Nyiragongo ulisababisha vifo vya watu 32 na kuacha maelfu bila makao ,Umoja wa Mataifa umesema.

Mlipuko huo mdogo wa hivi leo huenda ukazidisha hofu katika mji wa Goma ambao zaii ya nusu ya wakaazi wameondoka na waliobaki sasa watazingatia kuhamia maeneo ya mbali na sehemu zilizotajwa kama zilizopo kwenye hatari.Maelfu wameendelea kuondoka Goma lakini wakaazi wengine walikuwa wameanza kurudi.

Eneo hilo limepigwa na matetemeko ya ardhi zaidi ya 200 ambayo yameharibu majengo kadhaa, wakati nyufa mbili za urefu wa mita mia kadhaa zikionekana ardhini.

Goma ni mji wa ziwa ambapo watu karibu 670,000 wanaishi, kulingana na makadirio ya UN.

Ndima Kongba, Gavana wa kijeshi wa jimbo la Kivu Kaskazini, aliamuru kuhamishwa kwa karibu theluthi moja ya wakaazi wa jiji siku ya alhamisi akisema magma iligunduliwa chini ya Goma na Ziwa la Kivu lililo hapo karibu.

"Hivi sasa hatuwezi kuzuia mlipuko kwenye ardhi au chini ya ziwa," Bwana Kongba alisema, akiamuru wakaazi wa wilaya 10 za jiji kuhama.

Siku ya Ijumaa kulikuwa na dalili za maisha ya kawaida - maduka yalifunguliwa wazi, teksi za pikipiki zilikuwa zinafanya biashara yao - lakini unaweza kuhisi kuwa mambo sio jinsi yanavyopaswa kuwa.

Kwa wengine wa wale ambao hawakuondoka bado kuna hali ya hofu.