Uganda yaidhinisha dawa ya mitishamba kutibu corona

Dawa hiyo iliingia sokoni miezi kadhaa iliyopita.

Muhtasari

•Mamlaka ya udhibiti dawa nchini Uganda (NDA) imesema dawa hiyo imetengenezwa kwa mimea ambayo kwa asili inatumika kuondoa dalili za magonjwa kadhaa.

•Awali mamlaka ya NDA tarehe 14 mwezi Juni iliutahadharisha Umma dhidi ya matumizi ya Covidex ikisema kuwa haijaidhinisha uzalishaji wake, matumizi na mauzo kama tiba.

Virusi vya Korona
Virusi vya Korona
Image: Hisani

Uganda imeidhinisha matumizi ya dawa za mitishamba, Covidex kuwa dawa ya kusaidia kutibu ugonjwa wa Covid-19 na maambukizi mengine yanayosababishwa na virusi.

Mamlaka ya udhibiti dawa nchini Uganda (NDA) imesema dawa hiyo imetengenezwa kwa mimea ambayo kwa asili inatumika kuondoa dalili za magonjwa kadhaa.

Hatahivyo, dawa hiyo si ya kuponya ugonjwa wa Covid.

Maendeleo haya ni jitihada za mtengenezaji wake, Prof.Patrick Ogwang mtafiti mashuhuri wa dawa za mitishamba.

Awali mamlaka ya NDA tarehe 14 mwezi Juni iliutahadharisha Umma dhidi ya matumizi ya Covidex ikisema kuwa haijaidhinisha uzalishaji wake, matumizi na mauzo kama tiba.

Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbarara ambapo Prof Ogwang anafundisha kilisema kuwa dawa hiyo iliingia sokoni kimakosa kabla ya kufuatwa kwa taratibu zinazopaswa.

Sasa NDA inasema idhini ya sasa inategemea tathmini ya awali, chapisho la kisayansi, na usalama na kwamba mgunduzi pia alikuwa alikana madai yasiyothibitishwa kuwa bidhaa hiyo inatibu na inazuia covid-19.

Mamlaka pia imesema majaribio ya dawa hiyo yanapaswa kufanyika.

Dawa hiyo iliingia sokoni miezi kadhaa iliyopita.

Ilikuwa inauzwa kwa dola 0.84, lakini wakati maambukizi yakishika kasi kutokana na wimbi la pili la janga la corona, gharama yake imepanda na kufikia dola 22.5.

Watu 850,000 tu wamepewa chanjo, kipaumbele kikiwekwa kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, walimu, wazee, na wale walio na magonjwa nyemelezi.