HUKUMU YA ZUMA

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ajisalimisha mwenyewe kwa polisi

Usiku wa kuamkia leo umekuwa ni wa kwanza gerezani kwa Jacob Zuma, baada ya kujisalimisha mwenyewe kwa mamlaka husika jana usiku.

Muhtasari

•Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Rais huyo mstaafu ameamua kutii agizo la kufungwa kwake

•Baadhi ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba yake walielezea kutofurahishwa na kiongozi wao huyo kuhukumiwa kifungo gerezani.

JACOB ZUMA
JACOB ZUMA
Image: HISANI

Polisi nchini Afrika kusini imethibitisha kwamba aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma ametiwa nguvuni, baada ya kujisalimisha mwenyewe, ikiwa imepita wiki moja toka alipokutwa na hatia ya kuidharau Mahakama kufuatia kesi yake ya ufisadi na kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani.

Usiku wa kuamkia leo umekuwa ni wa kwanza gerezani kwa Jacob Zuma, baada ya kujisalimisha mwenyewe kwa mamlaka husika jana usiku.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Rais huyo mstaafu ameamua kutii agizo la kufungwa kwake.

Baada ya kufikia makubaliano ya kujisalimisha kwake na ujumbe wa Polisi uliofika nyumbani kwake mapema jana, Rais mstaafu wa Afrika kusini Jacob Zuma, akisindikizwa na walinzi wake alienda katika gereza lililokaribu na nyumbani kwake katika jimbo la KwaZulu Natal.

Baadhi ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba yake walielezea kutofurahishwa na kiongozi wao huyo kuhukumiwa kifungo gerezani.

Wafuasi wa Zuma waliadamana kupinga kukamatwa kwake
Wafuasi wa Zuma waliadamana kupinga kukamatwa kwake

Awali polisi ilitoa onyo la kutaka kumkamata Rais huyo mstaafu mwenye umri wa miaka 79, iwapo hatajisalimisha mwenyewe, ifikapo usiku wa jana.

Amehukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani, wiki iliyopita baada ya kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi ya rushwa iliyokuwa ikimkabili.

Zuma akipelekwa gerezani karibu na nyumbani kwake KwaZul-Natal
Zuma akipelekwa gerezani karibu na nyumbani kwake KwaZul-Natal

Hukumu dhidi ya Zuma ambayo ni ya kwanza dhidi ya Rais wa nchi, ilizua mtafaruku wa kisheria nchini Afrika kusini, huku muda wa mwisho ukiwekwa wa kujisalimisha usiku wa jana wa kukamatwa kwake.

Muda huo uliwekwa baada ya Rais Zuma kukataa kujisalimisha mwenyewe siku ya Jumapili.

Alishtakiwa kwa tuhuma za ufisadi katika kipindi cha miaka tisa ya uongozi wake madarakani. Tuhuma ambazo mwenyewe alizikana na kusema kuwa ni mhanga wa kisiasa.