Uporaji na vifo vyaongezeka katika purukushani zilizoanza kama maandamano ya kumuunga mkono Zuma

Muhtasari
  • Watu 30 waaga dunia kwenye Ghasia na uporaji Afrika Kusini
  • Lakini waandamanaji waligeuza maandamano hayo na kuwa ghasia mwishoni mwa wiki, wakichoma moto, kufunga barabara kuu na kuvamia na kupora maduka

Angalau watu 30 wamefariki kwenye ghasia zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini Afrika Kusini, tangu kujisalimisha kwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma wiki iliyopita.

Karibu watu 800 wamekamatwa katika ghasia hizo zilizoanza kama maandamano alhamisi iliyopita kupinga kwenda jela kwa Zuma.

Lakini waandamanaji waligeuza maandamano hayo na kuwa ghasia mwishoni mwa wiki, wakichoma moto, kufunga barabara kuu na kuvamia na kupora maduka.

Jeshi limepelekwa katika maeneo mbalimbali kuongeza nguvu na kusaidiana na Polisi kuzima ghasia hizo.

Waziri wa Polisi Bheki Cele amewaambia waandishi wa habari jana leo kwamba uporaji unaendelea na ipo hofu kwamba, kuna baadhi ya maeneo yatakuwa na uhaba wa bidhaa za msingi.

Wakati huo huo , Waziri wa ulinzi Nosiviwe Mapisa-Nqakula alisema hakuna haja ya kukiri kwamba nchi iko katika hali ya dharura kufuatia ghasia hizo katika majimbo ya KwaZulu-Natal na Gauteng.

Kiongozi wa KwaZulu-Natal Sihle Zikalala alisema watu 26 waliuawa katika jimbo hilo akiwemo kijana mdogo mwenye umri wa miaka 15, kwa mujibu wa ripoti ya EWN. Vifo sita vingine vimethibitishwa katika jimbo la Gauteng, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Maafisa wa serikali wanavilaumu vikundi vilivyoamua kutumia mgongo wa maandamano hayo ya kupinga kufungwa jela kwa Zuma kufanya vitendo vya jinai, wakati wengine wakitumia nafasi hiyo kuonyesha hasira zao kuhusu ukosefu wa ajira na umasikini hali inayochocheza zaidi ghasia hizo.

Lakini Bwana Cele ameonya 'hakuna kiwango chochote cha huzuni ama mazingira binafsi kutoka kwa watu wetu kinatoa haki ya kwa mtu yoyoter kupora, kuharibu na kuvunja sheria", alisema na kuongeza kuwa kwa sasa watu 12 wanachunguzwa kwa kuchochea ghasia hizo.

Inaelezwa kwamba zipo taarifa za kutungwa kwenye mitandao ya kijamii zinazochocheza ghasia hizo, huku chama tawala cha ANC kikisema kwmaba kinaendela kufuatitilia chapisho lililowekwa kwenye mtandao wa twitter na binti wa Zuma, Duduzile Zuma-Sambudla.

"Anatakiwa kujibu na kueleza chapisho lake lile lilikuwa na maana gani na linalenga nini," Jesse Duarte, katibu mkuu msaidizi wa chama hicho alisema, kwa mujibu wa gazeti la Daily Maverick la nchini humo.

Jana kiongozi wa upinzani wa chama cha EFF nchini humo, Julius Malema kupitia mtandao wake wa Twitter aliandika akisema, hawataki Polisi kutumika kudhibiti ghasia hizo, ni jambo la kisiasa linapaswa kushughulikiwa kisiasa.

Zuma alikutwa na hatia mwezi uliopita ya kushindwa kufika mahakamani wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya msingi inayomkabili ya vitendo vya rushwa wakati akiwa madarakani.

Rais huyo wa zamani anapinga kuhusika na vitendo vya rushwa na amehukumiwa miezi 15 kwenda jela, na alijisalimisha kwa Polisi jumatano iliyopita.

Anamatumaini kifungo hicho kinaweza kupunguzawa na mahakamani ya kikatiba ya nchi nhiyo, ingawa wanacheria wanaona iko nafasi finyu mno ya hilo kutokea.