Kiongozi wa upinzani Tanzania Freeman Mbowe aripotiwa kukamatwa

Bw Mbowe amedaiwa kukamatwa alipokuwa akihudhuria mkutano wa chama chake cha Chadema.

Muhtasari

•Maafisa kutoka chama chake wanasema kuwa hadi sasa hawajaweza kubaini anashikiliwa kwenye kituo kipi cha polisi.

•Mwanzoni mwa wiki hii kiongozi wa Chadema Freeman Mbowe alifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alilalamikia kukamatwa kwa wafuasi wa chama hicho na polisi, pamoja na suala la mabadiliko ya katiba.

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe ameripotiwa kukamatwa katika chumba chake cha hoteli jijini Mwanza.
Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe ameripotiwa kukamatwa katika chumba chake cha hoteli jijini Mwanza.
Image: CHADEMA

Kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe ameripotiwa kukamatwa katika chumba chake cha hoteli jijini Mwanza.

Bw Mbowe amedaiwa kukamatwa alipokuwa akihudhuria mkutano wa chama chake cha Chadema.

Hata hivyo polisi haijatoa tamko lolote kuhusiana na taarifa za kukamatwa kwake

Maafisa kutoka chama chake wanasema kuwa hadi sasa hawajaweza kubaini anashikiliwa kwenye kituo kipi cha polisi.

Kulingana na taarifa ya Chadema iliyotumwa kupitia akaunti yake ya Twitter, Bw Mbowe amekamatwa pamoja na wanachama wengine 10 wa chama hicho.

Kauli za hivi karibuni za Bw Mbowe

Mwanzoni mwa wiki hii kiongozi wa Chadema Freeman Mbowe alifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alilalamikia kukamatwa kwa wafuasi wa chama hicho na polisi, pamoja na suala la mabadiliko ya katiba.

Chama kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, CHADEMA kimesema hakitaendelea kumpigia magoti Rais wa nchi hiyo, Samia Hassan Suluhu kuhusu mustakabali wa taifa hilo, Bw Mbowe aliwaambia waandishi wa habari hivi Jumatatu.

Mwenyekititi huyo wa CHADEMA, aliyasema hayo kufuatia Jeshi la Polisi la nchi hiyo kuwakamata viongozi, wanachama wa chama hicho pamoja na viongozi wa dini 38 waliokuwa wahudhurie mkutano wa chama hicho kupitia baraza lake la vijana (BAVICHA) wenye lengo la kuhamasisha kupatikana kwa katiba mpya ya nchi hiyo.

Mara baada ya kuingia madarakani mwezi Machi mwaka huu, Rais Samia alitangazia umma dhamira yake ya kukutana na wapinzani ili kuzungumzia maswala mbalimbali ikiwemo ya kisiasa na namna gani ya kuendesha shughuli za siasa.

Licha ya kukutana na makundi mengine kama vijana, wazee na wanawake mpaka sasa Rais Samia hajakutaa na wapinzani. ‘‘Hatuwezi kuendelea na ule utaratibu wa zamani, tuna haki ya kukutana tunakamatwa, tunapigwa, tunashitakiwa, tunasoteshwa mahakamani miaka miwili miaka mitatu, kisha tunaachiwa huru, ama tunahukumiwa vifungo batili tukikata rufaa sote tunashinda’, alisema Mbowe

Pamoja na polisi kuzuia mkutano huo uliokua ufanyika kwenye ukumbi wa Hotel ya Boma wiki hii na kukamata watu hao 38, Kiongozi huyo wa Upinzani alisema, mkutano upo pale pale na utafanyika wiki hii na kama kukamatwa wako tayari kukamatwa wote.

Kama wanataka kuwaweka ndani wanachadema kwenye hoja hii ya katiba, wapanue kwanza na magereza, kwa sababu tuko tayari wote tuwekwe ndani , na wala hatutaomba dhamana’ alisema Mbowe kabla ya kulaani kitendo cha Jeshi la Polisi Mwanza, kuwakamata viongozi wa dini na wafuasi wa chama hicho .