Tanzania yaanza zoezi la kusambaza chanjo, kufikia walengwa nchi nzima

Muhtasari
  • Tanzania yaanza zoezi la kusambaza chanjo, kufikia walengwa nchi nzima

Serikali ya Tanzania imeanza zoezi la kusambaza chanjo kwenye mikoa yote ya nchi hiyo, baada ya kujiridhisha kuhusu ubora na usalama wa chanjo hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya nchi hiyo, iliyotolewa na Katibu mkuu wake, Profesa Abel Makubi imesema usambazaji huo unafanywa na wizara hiyo,

Uhakiki wa ubora na usalama wa chanjo hizo ya za Janssen kutoka Kampuni ya Johnson & Johnson nchini Marekani, umefanywa na mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA), Maabara ya Mkemia Mkuu, Maabara kuu ya Taifa na Vyombo vingine.

Baada ya usambazaji huo, inategemewa chanjo kuanzia kutolewa kwa makundi yaliyolengwa kuanzia Jumanne ya Agosti 3, 2021, kupitia vituo 550 vya kutolea huduma katika mikoa yote ya Tanzania bara.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo si kila mwananchi atapatiwa chanjo katika hatua ya sasa, bali kipaumbele ni kwa makundi yenye uhitaji mkubwa ambayo ni watumishi wa sekta ya Afya, watu wazima umri wa miaka 50 na kuendelea na watu wenye magonjwa.

Kama ilivyo kwa mataifa mengine wananchi watakaopatiwa chanjo watasajiliwa katika mfumo maalumu wa Taifa wa Chanjo na watapatiwa cheti baada ya kuchanjwa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kupitia mgao wa sasa wa chanjo kupitia mpango wa COVAX FACILITY, zitatolewa bure na kwa hiyari.

Nchi hiyo imepokea dozi za chanjo ya Johnson & Johnson zaidi ya milioni moja na uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo umefanyika wiki hii ukiongozwa na Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan.