Mtu aliyewauwa Polisi 2 Tanzania auawa

Wanaendelea kufuatilia kufahamu mtu huyo ametokea wapi na baadaye watatoa taarifa kamili.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi Nchini Simon Sirro, tukio hilo limetokea katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

• Rais Samia Suluhu ametoa salamu za rambirambi kwa familia za askari hao waliouawa pamoja na mlinzi wa kampuni ya SGA

Polisi wakipiga doria katika eneo la tukio
Polisi wakipiga doria katika eneo la tukio
Image: Reuters

Mtu mmoja aliyejihami kwa bunduki ameuawa baada ya kuwaua askari wawili katika majibizano ya risasi mkoani Dar es salaam.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi Nchini Simon Sirro, tukio hilo limetokea katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

“Mmeziona clip zinaruka sasa hivi akaingia barabara kubwa akawa anatamba na SMG na yeye amepigwa risasi na askari wetu hivyo, askari wetu wamefariki na yeye amefariki” IGP Sirro alinukuliwa akisema na gazeti la mwananchi nchini Tanzania..

Ameeleza kuwa wanaendelea kufuatilia kufahamu mtu huyo ametokea wapi na baadaye watatoa taarifa kamili.

Wakati huohuo Rais Samia Suluhu ametoa salamu za rambirambi kwa familia za askari hao waliouawa pamoja na mlinzi wa kampuni ya SGA aliyepoteza maisha yake .

Rais huyo amesema kwamba mtu huyo amedhibitiwa na kwamba hali imerudi kuwa shwari huku akiwataka polisi kufanya uchunguzi wa kina.

Awali Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa tahadhari ya dharura kufuatia kudhibitiwa kwa mtu huyo katika maeneo ya daraja la Salenda nje ya ubalozi wa Ufaransa nchini humo.

Mtu huyo aliyekuwa amejihami na bunduki aina ya AK 47 alikuwa amesimamia nje ya ubalozi huo huku akionekana kuyaelekeza magari yaliokuwa yakipitia barabara hiyo.

Hatahivyo polisi waliarifiwa na kumkabili jamaa huyo ambaye aliwaua maafisa wawili wa polisi .

Ubalozi huo umetoa wito kwa raia wake kuchukua tahadhari na kutotumia barabara ya tukio hilo.