• Inasemekana afisa huyo alikuwa amechukuwa mkopo wa shilingi laki tisa na pesa hizo zikachukuliwa na mpenziwe.
Maafisa wa jinai wamefanikiwa kumtia mbaroni afisa wa magereza aliyekuwa amedaiwa kutoroka kazini na bunduki kwa madai ya kumtafuta mpenziwe ili amuuwe.
Kulingana na idara ya DCI, Edwin Omuse anayehudumu katika gereza la Meru alikuwa ametishia kumuua mpenzi wake kwa madai kwamba alikuwa ametoroka na pesa zake shilingi laki tisa.
Afisa huyo alishikwa akiwa amejificha ndani ya nyumba ya mpenziwake akisubiri kumpiga risasi.
Imesemekana kwamba aliwasili mjini Thika ambapo mpenziwe aliishi na kuingia ndani ya nyumba yake kwa kutumia ufunguo wa ziada.
Akiwa katika nyumba ya mpenzi wake akimsubiri, maafisa wa upelelezi ambao walikuwa wanajua vizuri mpango huo walikuwa tayari wamemhamisha mwanamke huyo- aliyesemwa kuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya.
Kulingana na maafisa wa upelelezi, afisa huyo wa magereza alitayarisha bunduki ya G3 aliyokuwa amebeba kutoka Meru kwa gunia hadi Thika kutekeleza mauaji.
Wakati wa kukamatwa kwake, mshukiwa alikuwa na bunduki, ambayo ilikuwa na risasi 20.
Bunduki ilikuwa imefichwa chini ya kochi.
Kukamatwa kwake kulikuja baada ya ripoti kutolewa kwamba alikuwa ameonekana katika kituo cha kibiashara cha Kangeta na bunduki iliyofichwa kwenye gunia.
Polisi pia waliarifiwa kwamba alisikika akisema alikuwa akienda Thika kumuua mpenzi wake, ambaye alidai alimlaghai Ksh.900,000.
Inasemekana afisa huyo alikuwa amechukuwa mkopo wa shilingi laki tisa na pesa hizo zikachukuliwa na mpenziwe.