Polisi kushtakiwa kwa mauaji ya mwanafunzi wa sekondari

Muhtasari

• Sajenti John Otieno, ambaye alikuwa akihudumu katika kituo cha polisi cha Nyali, amepangiwa kuchukua kiapo cha kosa hilo.

• Uamuzi wa kushtakiwa ulifanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma baada ya kupitia ushahidi uliokusanywa na wachunguzi wa Ipoa.

Pingu
Image: Radio Jambo

Afisa wa polisi wa cheo sajenti atashtakiwa leo katika Mahakama Kuu ya Mombasa kwa mauaji ya mwanafunzi wa shule ya upili Tony Katana.

Katana aliuawa kwa kupigwa risasi katika Uwanja wa Mbuzi, Kongowea huko Mombasa mnamo Agosti 12, 2016.

Wakati wa kifo chake, Katana alikuwa na umri wa miaka 16, na mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Harvard huko Mombasa.

Aliuawa kwa kupigwa risasi katika tukio lililoshudiwa na maafisa wa polisi waliyokuwa kwenye doria pamoja na marafiki wa mwanafunzi huyo ambao walikuwa wameandamana naye kwenye harusi ya usiku katika eneo hilo.

Sajenti John Otieno, ambaye alikuwa akihudumu katika kituo cha polisi cha Nyali, amepangiwa kuchukua kiapo cha kosa hilo.

Kulingana na Mamlaka Huru ya Usimamizi wa Polisi (IPOA), tukio hilo lilipelekea kufanyika kwa uchunguzi baada ya mwili wa mwanafunzi huyo kugunduliwa na kutambuliwa na jamaa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali Kuu ya Pwani siku iliyofuata.

Mwenyekiti wa Ipoa Anne Makori alisema kuwa "kulingana na Sehemu ya 25 ya Sheria ya Ipoa vifo ambavyo ni matokeo ya hatua ya polisi au vilivyosababishwa na wanachama wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi wakiwa kazini vichunguzwe na mamlaka hiyo."

"Kwa hivyo, mamlaka ilianzisha uchunguzi ambao ulithibitisha mwanafunzi huyo alikufa kwa majeraha ya risasi yaliyosababishwa wakati wa makabiliano na polisi na kwamba kifo hicho kiko chini ya mamlaka ya Ipoa; kuwawajibisha polisi kwa matendo yao. ”

Uamuzi wa kushtakiwa ulifanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma baada ya kupitia ushahidi uliokusanywa na wachunguzi wa Ipoa.