Hasira zaibuka baada ya mgeni kuonyesha kwenye televisheni namna alivyobaka wanawake

Muhtasari

• Mgeni aliyeelezewa kama mbakaji wa zamani alionyesha kwa vitendo kwa kutumia mwanasesere jinsi alivyowadhalilisha wanawake.

Image: NCI

Kituo cha televisheni huko Ivory Coast kimeomba radhi baada ya kurusha kipindi ambapo mgeni aliyeelezewa kama mbakaji wa zamani alionyesha kwa vitendo kwa kutumia mwanasesere jinsi alivyowadhalilisha wanawake.

Mtangazaji huyo alicheka na kuzungumza kwa utani wakati akimsaidia mgeni kuweka mwanasesere kwenye sakafu. Baadaye mgeni huyo alialikwa kutoa ushauri kwa wanawake juu ya jinsi ya kuepuka kubakwa.

Watu elfu thelathini walisainimalalamiko wakitaka kufutwa kwa kipindi hicho cha chaneli binafsi ya Nouvelle Chaîne Ivoirienne (NCI).

Waziri wa masuala ya wanawake Nassénéba Touré alikuwa miongoni mwa watu walioonesha kughadhibishwa, akisema kipindi cha Jumatatu kimedhoofisha juhudi za kupambana na vitendo vya ubakaji

Mtangazaji, Yves de M'Bella, amesimamishwa kazi na ameomba radhi.

Uongozi wa kituo hicho umesema unazingatia kuheshimu haki za binadamu, hasa za wanawake.