Uganda kuwachanja watu milioni 6 kabla ya shule kufunguliwa mwakani

Muhtasari

Sekta ya elimu itafunguliwa tena mnamo Januari 2022, isipokuwa vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu, ambazo zitafunguliwa kutoka Novemba 1.

Museveni
Rais Yoweri Museveni Museveni

Uganda inakusudia kuchanja watu wasiopungua milioni sita ifikapo mwisho wa mwaka, kabla ya shule kufunguliwa.

Karibu watu milioni 4.8 ya hao wameorodheshwa kama kipaumbele cha juu, na ni pamoja na wafanyikazi wa afya, walimu, wanafunzi wenye umri wa miaka 18 na zaidi, na wafanyikazi wa usalama kati ya wengine.

Sekta ya elimu itafunguliwa tena mnamo Januari 2022, isipokuwa vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu, ambazo zitafunguliwa kutoka Novemba 1.

Shule zilifungwa kwa mara ya kwanza mnamo Machi 2020, zikafunguliwa kwa muhula wa mwisho wa mwaka, lakini zikafungwa tena mnamo Juni mwaka huu wakati wimbi la pili la janga la Coron lilipokumba taifa hilo

Katika hotuba ya kitaifa iliyopeperushwa kwa njia ya televisheni Jumanne, Rais Yoweri Museveni alisema kuwa kuna dozi za chanjo milioni 2.2 za Covid 19 zinazopatikana nchini kwa sasa, na wastani wa milioni kumi zaidi zinatarajiwa kuwasili katika miezi ijayo.

Tangu dozi za kwanza zifike Uganda mnamo Machi, ni watu 600,000 tu wamepewa chanjo kamili nchini humo.