Kiongozi wa kijeshi wa Guinea kuapishwa kuwa rais

Muhtasari

• Sherehe ya kuapishwa kwake itafanyika katika ikulu ya rais na itahudhuriwa na wale walioalikwa pekee.

Kiongozi wa kijeshi nchini Guinea Kanali Mamady Doumbouya anatarajiwa kuapishwa leo kama rais wa mpito.

Sherehe ya kuapishwa kwake itafanyika katika ikulu ya rais na itahudhuriwa na wale walioalikwa pekee.

Kanali Doumbouya aliongoza mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Rais Alpha Condé mapema mwezi uliopita.

Anatarajiwa kuunda serikali katika wiki chache zijazo.

Kiongozi huyo wa kijeshi aliye na miaka 41, atakuwa kiongozi wa pili wa Afrika mwenye umri mdogo kuongonza nchi, mdogo zaidi akiwa ni wa Mali Kanali Assimi Goïta, 38 ambaye aliongoza mapinduzi ya kumng’oa madarakani Rais Keïta.

Baada ya mapinduzi ya Guinea Kanali Doumbouya alisema askari wake wamechukua uongozi na walitaka kumaliza ufisadi, ukiukwaji wa haki za binadamu na usimamizi mbaya uliokithiri nchini humo.

Rais Condé alichaguliwa katika uchaguzi uliokumbwa na utata kuongoza kwa muhula wa tatu licha ya maandamano ya ghasia mwaka jana.