Unyanyasaji wa kingono: Maelfu walilawitiwa kanisani Ufaransa, uchunguzi wasema

Muhtasari

•Jean-Marc Sauvé ameviambia vyombo vya habari vya Ufaransa kuwa kamati ya uchunguzi imebaini ushahidi wa unyanyasaji uliotekelezwa kati ya wanyanyasaji 2,900 hadi 3,200 - miongoni mwa jumla ya mapadre 115,000 na viongozi wengine wa kidini.

•Uchunguzi huo uliitishwa na Kanisa Katoliki nchini Ufaransa katika mwaka 2018, kufuatia kashfa kadhaa katika mataifa mengine.

Image: GETTY IMAGES

Maelfu ya walawiti wamekuwa wakifanya ulawiti ndani ya Kanisa katoliki la Ufaransa tangu mwaka 1950, mkuu wa jopo la uchunguzi kuhusu unyanyasaji uliofanywa na wajumbe wa kanisa anasema.

Jean-Marc Sauvé ameviambia vyombo vya habari vya Ufaransa kuwa kamati ya uchunguzi imebaini ushahidi wa unyanyasaji uliotekelezwa kati ya wanyanyasaji 2,900 hadi 3,200 - miongoni mwa jumla ya mapadre 115,000 na viongozi wengine wa kidini.

"Hayo ni makadirio ya chini," aliongeza.

Kamati hiyo inatarajiwa kutoa ripoti ndefu Jumanne. Ripotihiyo imetokana na taarifa zilizopatikana kutoka kwenye makumbusho ya Kanisa, mahakama na polisi, pamoja na mahojiano na waathiriwa wa unyanyasaji huo.

Uchunguzi huo uliitishwa na Kanisa Katoliki nchini Ufaransa katika mwaka 2018, kufuatia kashfa kadhaa katika mataifa mengine.

Bw Sauvé, ambaye ni mfanyakazi wa umma wa ngazi ya juu nchini Ufaransa, ameliambia gazeti la Ufaransa Le Monde kwamba jopo analoliongoza lilikuwa limewasilisha ushahidi kwa waendesha mashitaka katika kesi 22 ambazo mashitaka ya uhalifu bado yanaweza kuanzishwa.

Aliongeza kuwa maaskofu na maafisa wengine wa ngazi ya juu walikuwa wamefahamishwa kuhusu madai mengine dhidi ya watu ambao bado wanaishi.

Wajumbe wa kamati hiyo ya uchunguzi walikuwa ni pamoja na wanahistoria, madaktari na wanatheolojia.

Zaidi ya waathiriwa 6,500 na mashahidi waliwasiliana na tume hiyo katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita. Ripoti ya mwisho ya uchunguzi huo ina jumla ya kurasa 2,500.