Kaohsiung: Moto katika jengo la gorofa Taiwan waua takriban watu 46

Muhtasari
  • Takriban watu 46 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa vibaya katika mkasa wa moto uliotokea kwenye jengo la ghorofa 13 la kusini mwa Taiwan, maafisa wanasema

Takriban watu 46 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa vibaya katika mkasa wa moto uliotokea kwenye jengo la ghorofa 13 la kusini mwa Taiwan, maafisa wanasema.

Jengo la makazi na biashara katika mji wa Kaohsiung liliteketea moto asubuhi ya Alhamisi, idara ya zima moto ilisema.

Iliwachukua wazima moto zaidi ya saa nne kuzima moto huo.

Idara ya zimamoto iliambia BBC kuwa watu 79 walipelekwa hospitalini, wakiwemo 14 katika hali mbaya.

Sababu ya moto haijulikani na wachunguzi wako katika eneo la tukio.

Maafisa mapema walionya kwamba watu wanaweza kuwa wamenaswa katika sehemu ya makazi ya jengo hilo, kati ya sakafu ya gorofa ya saba na ya 11.

Wakazi wa karibu waliambia vyombo vya habari vya huko walisikia kishindo kikubwa ambacho kilisikika kama mlipuko kabla ya moto.

Kwingine ni kuwa;

Mshukiwa wa shambulio la mishale na uta akamatwa Norway

 

Mwanaume mmoja amekamatwa akihusishwa na shambulio la mishale na uta lililotokea nchini Norway .

Na kulikuwa na hofu kuwa alikuwa anaendeleza shambulizi, polisi imesema.

Mwanaume huyo ambaye ana umri wa miaka 37-mwenye uraia wa Denmark anashutumiwa kuua wanawake wanne na mwanaume mmoja siku ya Jumatano huko kusini mwa mji wa Kongsberg.

Kamanda mkuu wa polisi wa Ole Bredrup Saeverud alisema maofisa waliwahi kukutana na mwanaume huyo mwaka jana .

Alikamatwa na kuhojiwa maswali kadhaa majira ya usiku.

Waathirika wa shambulio hilo walikuwa na umri wa kati ya 50 na 70, mkuu wa polisi Saeverud aliwaambia waandishi Alhamisi asubuhi.

Polisi walimkamata mshambuliaji huyo dakika sita baada ya shambulio kutokea siku ya Jumatano lakini alitoroka na kukamatwa tena baada ya dakika 35 baada ya shambulio kutokea.

Polisi wanasema inawezekana watu wote aliowauwa waliuliwa mara baada ya polisi kukabiliana naye mara ya kwanza.