Jeshi la Sudan lavunja serikali ya kiraia na kuwakamata viongozi

Muhtasari

• Jenerali Abdel Fattah Burhan, ambaye alikuwa akiongoza baraza la pamoja na viongozi wa kiraia, alilaumu mapigano ya kisiasa kwa hatua hiyo.

•Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ni miongoni mwa wale walioripotiwa kuzuiliwa nyumbani.

Jeshi la Sudan limevunja utawala wa kiraia, limewakamata viongozi wa kisiasa na kutangaza hali ya hatari.

Jenerali Abdel Fattah Burhan, ambaye alikuwa akiongoza baraza la pamoja na viongozi wa kiraia, alilaumu mapigano ya kisiasa kwa hatua hiyo.

Waandamanaji wameingia kwenye barabara za mji mkuu, Khartoum, na kuna ripoti za milio ya risasi .

Viongozi wa jeshi na raia wamekuwa wakipingana tangu kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir kupinduliwa miaka miwili iliyopita na serikali ya mpito kuanzishwa.

Waziri Mkuu Abdallah Hamdok ni miongoni mwa wale walioripotiwa kuzuiliwa nyumbani.

Picha za video kutoka mji mkuu wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika Jumatatu zilionyesha waandamanaji wakisimamia vizuizi karibu na makao makuu ya jeshi.

Taarifa kutoka kwa wizara ya habari kwenye Facebook ilisema kuwa kukamatwa kwa viongozi hao kulitekelezwa na "vikosi vya jeshi vya pamoja" na wale waliokamatwa walikuwa wakishikiliwa "mahali pasipojulikana".

Wizara hiyo ilisema askari walishambulia Makao Makuu ya shirika la utangazaji la serikali, huko Omdurman, na kuwazuia wafanyikazi hapo.

Pia ilisema Bw Hamdok alikuwa akishinikizwa kuunga mkono mapinduzi lakini alikuwa akikataa kufanya hivyo na aliwahimiza watu waendelee na maandamano ya amani "kutetea mapinduzi".

Mjumbe maalum wa Uingereza kwa Sudan na Sudan Kusini, Robert Fairweather, alisema kupita Twitter kwamba kukamatwa kwa viongozi wa raia itakuwa "usaliti wa mapinduzi, mpito na watu wa Sudan".

Mashahidi wanasema mawasiliano ya mtandao yamekatishwa na kwamba jeshi na vikosi vya kijeshi vimepelekwa kote jijini. Uwanja wa ndege wa Khartoum sasa umefungwa, na safari za ndege za kimataifa zimesimamishwa.

Unachofaa kujua

Mapinduzi ambayo yanaonekana kuendelea nchini Sudan ni mzozo wa hivi karibuni katika kipindi cha machafuko kwa nchi hiyo.

Awamu hii ni matokeo ya kutoaminiana kati ya viongozi wa kijeshi na raia.

Wamekuwa wakigawana madaraka tangu Agosti 2019 kufuatia kupinduliwa kwa Rais Omar al-Bashir aliyehudumu kwa muda mrefu mapema mwaka huo.

Alipinduliwa na wanajeshi lakini maandamano ya kila mara ambayo hayakuwahi kutokea yalilazimisha wanajeshi kujadili mpango uliolenga kuhamia serikali ya kidemokrasia.

Nchi sasa inapaswa kuwa katika mpito huo na raia na viongozi wa jeshi wanaoendesha nchi pamoja kwenye kamati ya pamoja inayojulikana kama Baraza Kuu.

Lakini vikundi hivyo viwili vimekuwa vimepingana hadharani.

Kiongozi mkuu wa kiraia , Waziri Mkuu Abdallah Hamdok, sasa ameripotiwa kuzuiliwa na wanajeshi, pamoja na mawaziri wengine kadhaa. Inaonekana pia kwamba makao makuu ya Runinga na redio yamechukuliwa na jeshi.

Mtandao pia umezuiliwa.

Jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwezi uliopita lilizidisha mvutano.

Na katika wiki za hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia maandamano yakitaka jeshi lichukue madaraka pamoja na maandamano makubwa yanayomuunga mkono waziri mkuu.

Waandamanaji wanaounga mkono jeshi wameishutumu serikali kwa kushindwa kufufua utajiri wa nchi hiyo wakati uhaba wa mkate ukizidi .

Hatua za Bwana Hamdok za kurekebisha uchumi - pamoja na kuounguza ruzuku ya mafuta - hazijapendwa na wengine.

Kulingana na ukurasa wa Facebook wa wizara ya habari, waziri mkuu sasa ametoa wito kwa watu kujitokeza kuunga mkono serikali.

Picha na ripoti zingine zinazotoka katika mji mkuu, Khartoum, zinaonyesha kwamba kuna waandamanaji nje ya jiji.

Wanajeshi pia wametumwa kuzuia usafiri wa watu kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Mnamo Juni 2019, kabla ya mabadiliko ya kidemokrasia kukubaliwa, wanajeshi waliwafyatulia risasi waandamanaji huko Khartoum na kuua watu wasiopungua 87.

Kumbukumbu za mauaji hayo zitakuwa zikijirudia kwenye akili za watu wakati pande hizo mbili zikikabiliana.