Mzozo wa Tigray ni hatari kwa uwekezaji Ethiopia-Safaricom

Muhtasari
  • Safaricom pia haina dhamana ya mkopo wa dola milioni 500 kutoka kwa Shirika la Fedha la Maendeleo la Marekani
  • Serikali ya Marekani katika siku za hivi karibuni iliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Ethiopia, ikitaja ukiukaji wa haki za binadamu

Safaricom, ambayo ni kampuni kubwa na yenye faida kubwa zaidi ya kutoa huduma za mawasiliano katika Afrika Mashariki na Kati imethibitisha kuwa imewahamisha wafanyakazi na wanakandarasi kutoka Ethiopia, kutokana na kukithiri kwa ukosefu wa usalama wiki kadhaa baada ya Ethiopia kutangaza hali ya hatari kutokana na vita vinavyoendelea huko Tigray, kaskazini mwa Addis Ababa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Peter Ndegwa, hata hivyo ana matumaini ya huduma nchini Ethiopia ambako ilishinda leseni ya kutoa huduma za simu za mkononi ambayo itazinduliwa katikati ya mwaka 2022 mara tu miundombinu yote itakapowekwa.

Uchunguzi wa moja kwa moja na BBC, Jumatano asubuhi, mjini Addis Ababa ulikuta shughuli chache katika ofisi ya kampuni hiyo, na dalili zote kwamba mustakabali wa haraka haujulikani.

Safaricom pia haina dhamana ya mkopo wa dola milioni 500 kutoka kwa Shirika la Fedha la Maendeleo la Marekani.

Serikali ya Marekani katika siku za hivi karibuni iliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Ethiopia, ikitaja ukiukaji wa haki za binadamu.

Miongoni mwa vikwazo ni, kufuta makubaliano ya biashara ya upendeleo ya Ethiopia kwa mauzo ya nje bila ushuru kwenda Marekani (AGOA).

Ethiopia iliuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 237 chini ya makubaliano ya Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika mwaka 2020 pekee.

Kampuni hiyo inaongoza muungano unaojumuisha Sumitomo Group ya Japan, Vodacom na wakala wa maendeleo wa Uingereza, CDC Group kwa ufadhili wa Shirika la Fedha la Maendeleo la Marekani na tangu wakati huo imeanzisha kampuni ya uendeshaji mjini Addis Ababa yenye mpango wa kuwekeza dola bilioni 2 na kuajiri watu wapatao 1,000 kwa miaka mitano ya kwanza.