Wapenzi wafungwa miaka 2 kwa kula uroda hadharani

Muhtasari

•Wiki iliyopita video ya wawili hao wakishiriki tendo la ndoa barabarani mchana kweupe pe! huku kukiwa na rasharasha za mvua  ilisambazwa kote mitandaoni.

•Mukamulenzi alisema alikubali kitendo hicho baada ya jamaa kuahidi kulipa shilingi mia tano za Uganda.

Mahakama
Mahakama

Wapenzi wawili kutoka nchi jirani ya Uganda watahudumu kifungu cha miaka miwili unusu kwa kula uroda hadharani.

Mwendesha bodaboda Hafashimana Paskari (29) na Muhawenimana Colodine Mukamulenzi (24) kutoka wilaya ya Kisoro  walifikikishwa katika mahakama ya Kisoro siku ya Jummanne na kushtakiwa kwa kosa la kusababisha kero kwa umma.

Wawili hao walikamatwa wiki iliyopita baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini humo kuagiza washtakiwe kwa kitendo hicho kisichofaa.

Wiki iliyopita video ya wawili hao wakishiriki tendo la ndoa barabarani mchana kweupe pe! huku kukiwa na rasharasha za mvua  ilisambazwa kote mitandaoni.

Kwenye video hiyo, Paskari na Mukamulenzi walionekana wakitembea kwenye barabara moja ya lami kisha wakasimama na kuanza mchezo wa kitandani bila kujali macho zilizokuwa zinawatazama.

Kufuatia hayo wawili hao walikamatwa na kufikishwa mahakamani ambako walikubali mashtaka dhidi yao.

Ilidaiwa mnamo Novemba 2, 2021 mwendo wa saa kumi na moja jioni, Paskari na Mukamulenzi walishiriki mapenzi hadharani katika barabara ya Kisoro.

Mukamulenzi alisema alikubali kitendo hicho baada ya jamaa kuahidi kulipa shilingi mia tano za Uganda.

Hakimu Fred Gidudu aliwahukumu wapenzi hao kifungo cha miezi 30 gerezani.