Rais Kagame: 'Tutaingilia popote ili kulinda amani na Usalama'

Muhtasari

• "Ni dhamira yetu kupambana na ugaidi na kuwalinda raia popote tunapoitwa, ni jambo ambalo tunaliamini na tumepitia." Msemaji wa jeshi la Rwanda aliiambia BBC baada ya kutumwa nchini Msumbiji.

Rais Kagame wa Rwanda
Rais Kagame wa Rwanda
Image: GETTY IMAGES

Rwanda, baada ya kupitia misuko siku ya mauaji ya kimbari, "sasa imejitolea kuchukua hatua popote inapohitajika ili kuleta amani na usalama", kauli ya Rais Paul Kagame wa nchi hiyo.

Suala hilo la amani ndio limekuwa msukumo wa hatua ya nchi hiyo kuingilia kati mizozo katika nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Msumbiji baada ya makubaliano kati ya serikali ya nchi hizo na Rwanda.

Baada ya kupigana katika vita vikali vya hivi karibuni vya kikanda nchini Rwanda, DR Congo, au kaskazini mwa Angola mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, majeshi ya Rwanda leo yanafahamika kwa uzoefu wao, mafunzo ya mara kwa mara, vifaa vya kutosha na nidhamu.

"Ni dhamira yetu kupambana na ugaidi na kuwalinda raia popote tunapoitwa, ni jambo ambalo tunaliamini na tumepitia." Msemaji wa jeshi la Rwanda aliiambia BBC baada ya kutumwa nchini Msumbiji.

Sifa ilizozipata nchi hiyo kwenye misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimevifanya vikosi vya Rwanda kuwa miongoni mwa vikosi vyenye mchango mkubwa duniani katika misheni hizo.

Image: REUTERS

Hata hivyo, uingiliaji kati wa hivi majuzi nchini CAR na Msumbiji umekosolewa na wanachama wa upinzani wa ndani kwa sababu ya kutowekwa wazi kwa "makubaliano" yaliyoko.

Rwanda ilikubali kufadhili kikamilifu "uingiliaji kati wake" katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji, jambo ambalo liliibua maswali kutoka kwa upinzani "kwa nini Rwanda inafadhili vita ghali kwenye nchi ya Msumbiji ambayo ni tajiri?(kwa mujibu wao wakilinganisha Rwanda na Msumbiji)", mwanasiasa mfungwa Christopher Kayumba alihoji mwezi Julai wakati vikosi vya jeshi vya Rwanda vilipokuwa vinaenda Msumbiji.

Pamoja na yote, Rwanda kuingilia mzozo huo wa Msumbiji na hata ule wa nchini CAR umeipatia sifa nchi hiyo katika kupambana na ugaidi nchini Msumbiji na kulinda serikali inayoanguka Bangui.

Kampeni hizo zinaifanya Rwanda kuwa mhusika mkuu katika siasa za kikanda na inaweza kuifanya nchi hiyo kuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya ugaidi barani Afrika na duniani kote.

Rais Kagame (kushoto) na mwenyeji wake Rais wa Msumbiji, Nyusi, alipofanya ziara kwenye jimbo laCabo Delgado mwezi Septemba, baada ya kuwasili katika eneo hilo karibu wanajeshi 1,000 wa Rwanda
Rais Kagame (kushoto) na mwenyeji wake Rais wa Msumbiji, Nyusi, alipofanya ziara kwenye jimbo laCabo Delgado mwezi Septemba, baada ya kuwasili katika eneo hilo karibu wanajeshi 1,000 wa Rwanda
Image: GETTY IMAGES

Mizozo katika nchi za Msumbiji na CAR

Kwa muda mrefu sasa tangu mwaka 2017 Msumbiji imekuwa eneo maarufu zaidi linalokumbwa na ugaidi kusini mwa Afrika. Vitendo vya utekaji nyara, kukata vichwa, na kuchoma nyumba vimekuwa vitendo vya kundi la siri la waasi huko Cabo Delgado, Kaskazini mwa Msumbiji.

Tangu mwaka huo kumekuwa na uvamizi na kusababisha idadi isiyojulikana ya vifo na kulazimisha zaidi ya watu 700,000 kukimbia makazi yao ili kuyanusuru maisha yao. Mpaka sasa sababu halisi za uasi hazijulikani, ingawa suala la rasilimali iliyopo eneo la Cabo Delgado inatajwa kama chanzo, lakini hakuna anayeweza kuthibitisha moja kwa moja.

Nchi ya CAR yenyewe imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa kikabila pamoja na ule wa kidini tangu 2013. Kundi la Seleka lilishikilia mamlaka kwa muda mwezi Machi 2013 na kumng'atua mamlakani rais Mkristo Francois Bozize.

Waasi hao baadaye walitimuliwa na kusababisha ghasia dhidi ya Waislamu walio wachache hatua iliyochukuliwa na wapiganaji wa kundi la kikristo la anti-Balaka.

Pengine ni jambo la kusubiri kuona kama hatua ya Rwanda kuingilia mizozo hii katika nchi hizi mbili ili kuleta amani na kudumisha silaha inaweza kufua dafu.