Mwanawe Gaddafi kugombea kiti cha urais Libya

Muhtasari
  • Tangu kuibuka kwa maandamano ya mwaka 2011 ya kupinga serikali, Libya imekumbwa na mzozo
Image: BBC

Mwana wa kiume wa marehemu kiongozi wa Libya Muammar al-Gaddafi amejisajili kama mgombea wa kwanza wa urais wa moja kwa moja katika uchaguzi wa urais wa mwezi ujao.

Saif al-Islam Gaddafi wakati mmoja alitarajiwa kuwa mrithi wa baba yake, lakini hatua yake ya kuunga mkono msakao wa kikatili dhidi ya waandamanaji mika 10 iliyopita ilimchafulia sifa.

Tangu kuibuka kwa maandamano ya mwaka 2011 ya kupinga serikali, Libya imekumbwa na mzozo.

Makundi ya kutetea haki yameelezea wasiwasi wao kuhusu uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Disemba 24, ikiwa utakuwa huru na wa haki.

Nchi zenye uwezo mkubwa duniani na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga au kufanya udanganyifu atakabiliwa na vikwazo.

Picha na video zinazosambazwa mitandaoni zinamuonesha Saif al-Islam Gaddafi akiwa kwenye bango la uchaguzi, akisaini makaratasi ya uchaguzi.

Akiwa na ndevu na mavazi ya kitamaduni ya Libya, alihutubia kwa kunukuu aya za Quran zilizotafsiriwa kama, "hukumu baina yetu na watu wetu kwa haki".

"Mungu daima anashinda katika kusudi lake," alisema pia, akinukuu sura nyingine ya kitabu kitakatifu cha Waislamu, na kuongeza kutoka sehemu nyingine - "hata kama makafiri wanachukia".

Ni taswira tofauti kabisa na ile aliyoitoa kabla ya ghasia zilizomwangusha babake mwaka wa 2011.

Baada ya mwisho wa utawala wa kikatili wa Muammar Gaddafi, Saif al-Islam Gaddafi mwenyewe alikamatwa na wanamgambo.

Alizuiliwa kwa miaka sita, kupewa hukumu ya kifo ambayo baadaye ilibadilishwa

Bw Gaddafi bado anatafutwa kwa mashtaka ya uhalifu wa kivita na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, lakini hatua kwa hatua amejitokeza tena hadharani, ikiwa ni pamoja na kupitia mahojiano na New York Times kutoka kwenye jumba lake la kifahari huko Zintan mapema mwaka huu.

Saif al-Islam Gaddafi: Mwana wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya kugombea urais

'Mgawanyiko lakini sio ajabu'

Kurejea kwa Bw Gaddafi kumepokelewa kwa hisia mseto kwa kiasi kikubwa nchini Libya, anasema mwandishi wa BBC Monitoring Amira Fathalla. Bado kuna ati ati katika azma yake ya uongozi, kwani amekuwa akitajwa mara kwa mara kama mgombea kwa miaka.

Kumbukumbu nchini Libya bado ni mbichi sana kwake kushinda urais, anasema mhariri wa BBC Mashariki ya Kati Sebastian Usher, na kugombea kwake kutatatanisha zaidi mchakato wa uchaguzi ambao tayari ni dhaifu.

Baada ya miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na madola hasimu yanayoendesha shughuli zake mashariki na magharibi mwa nchi, Libya kwa sasa inaongozwa na serikali ya mpito lakini bado haijayumba kisiasa.

Kutokuelewana kati ya vyombo vya kisiasa vya Libya na pande zinazopingana kuhusu sheria za uchaguzi na ratiba kumetishia kuvuruga kura ya urais.

Wagombea wengine katika kinyang'anyiro hicho ni mbabe wa kivita Khalifa Haftar - ambaye hapo awali aliongoza uasi kutoka kambi yake ya mashariki dhidi ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli, pamoja na Waziri Mkuu Abdulhamid al-Dbeibah na spika wa bunge Aguila Saleh.