Wanajeshi wawili wa Uganda wahukumiwa kifo Somalia

Wamepatwa na hatia ya kuwaua raia saba nchini humo.

Muhtasari

•Wawili kati ya wanajeshi hao wamehukumiwa kifo, huku wengine watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 39 gerezani kila mmoja.

•Karibu theluthi ya jeshi la Amisom lenye maafisa 20,000 wanatoka Uganda- likiwa ni sehemu kubwa ya jeshi kuliko wanaotoka nchi nyingine.

Image: AFP

Wanajeshi watano wa Uganda wanaofanya kazi na vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia wamepatwa na hatia ya kuwaua raia saba nchini humo.

Wawili kati ya wanajeshi hao wamehukumiwa kifo, huku wengine watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 39 gerezani kila mmoja.

Wanajeshi hao watatu watarudishwa Uganda ili kutumikia vifungo vyao.

Raia hao waliuawa kinyume cha sheria wakati wa mapigano ya risasi huko Golweyn kati ya wanajeshi wake na wanamgambo wa al-Shabab, AU inasema.

Jeshi la Amisom la Umoja wa Afrika limekuwepo Somalia kwa miaka 14.

Limekuwa likipambana na wanamgambo wa Kiislamu wa al-Shabab ambao wanashikilia sehemu ya nchi hiyo.

Karibu theluthi ya jeshi la Amisom lenye maafisa 20,000 wanatoka Uganda- likiwa ni sehemu kubwa ya jeshi kuliko wanaotoka nchi nyingine.

Uamuzi wa mahakama ya kijeshi wa Jumamosi wa Uganda unakuja mwezi mmoja baada ya AU kutangaza kutaka kupanua operesheni yake ya kijeshi nchini Somalia, ikisubiri kibali kutoka kwa Umoja wa Mataifa na serikali ya Somalia.

"Dhamira yetu nchini Somalia ni kudhalilisha al-Shabab na makundi mengine yenye silaha. Kwa kufanya hivyo, tuna kila jukumu la kulinda raia," alisema kamanda wa kikosi cha Uganda Brigedia Jenerali Don Nabasa katika taarifa yake Jumamosi.

VOA inaripoti kuwa baadhi ya familia za waathiriwa walihudhuria vikao vya mahakama vilivyoandaliwa na Uganda katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

"Tumefurahishwa sana na uamuzi wa mahakama na tunatarajia fidia itatolewa kwa familia za waliouawa," Hussein Osman Wasuge - msemaji wa jamaa wa marehemu - alinukuliwa akisema.