Waathiriwa wa milipuko ya Uganda watibiwa katika hospitali ya Kampala - ripoti

Muhtasari
  • Waathiriwa wa milipuko ya Uganda watibiwa katika hospitali ya Kampala
  • Moja ya milipuko hiyo ilitokea karibu na Kituo Kikuu cha Polisi katika wilaya kuu ya kibiashara ya Kampala
Image: BBC

Wodi ya majeruhi ya hospitali kuu katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, imejaa watu waliojeruhiwa katika milipuko ya asubuhi, tovuti ya habari ya Independent inaripoti.

Inasema wengi wa waliojeruhiwa ambao walikuwa wameletwa katika Hospitali ya Mulago kwa magari ya wagonjwa ni maafisa wa polisi.

Moja ya milipuko hiyo ilitokea karibu na Kituo Kikuu cha Polisi katika wilaya kuu ya kibiashara ya Kampala.

Kituo cha runinga cha NTV kimezungumza na daktari katika kituo kingine cha afya ambaye alisema walipokea majeruhi 17. Kumi na wawili walishauriwa kwenda Mulago huku wengine watano wakirudishwa nyumbani.

Ubalozi wa Marekani ulikuwa umeonya kuhusu mashambulizi zaidi nchini Uganda

Ubalozi wa Marekani mjini Kampala, Uganda ulikuwa umeonya kuhusu "uwezekano wa mashambulizi zaidi ya kigaidi nchini Uganda", wiki tatu zilizopita.

Onyo hilo lilikuwa katika tahadhari ya usalama ya tarehe 26 Oktoba.

Tahadhari hiyo ilitolewa baada ya milipuko mingine miwili mjini Kampala, ambapo kundi la wanamgambo lilidai kutekeleza.

Ubalozi huo uliwaonya raia wa Marekani wakati huo "kukaa macho na kufahamu mazingira yao wanaposafiri nchini Uganda"