Saif Gaddafi azuiwa kugombea urais Libya

Muhtasari
  • Bw Gaddafi aliibua utata baada ya kutangaza kwamba atagombea urais
  • Watu sitini waliwasilisha maombi ya kugombea urais wa Libya kufikia Jumatatu
Image: BBC

Mwana wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa Libya hayati Muammar Gaddafi ameenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania uchaguzi wa tarehe 24 Disemba.

Tume ya uchaguzi ilikataa maombi kadhaa ya kugombea kiti hicho yakiwemo ya Saif al-Islam Gaddafi, ikitaja "sababu za kisheria", vyombo vya habari viliripoti.

Bw Gaddafi aliibua utata baada ya kutangaza kwamba atagombea urais.

Anasakwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa madai ya uhalifu wa kivita na mauaji wakati baba yake alipoongoza taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Maombi ya kuwania urais ya mwanasiasa mwenye ushawishi Khalfa Haftar pia yalisababisha wasiwasi katika nchi hiyo, kwani anakabiliwa na mashitaka katika mahakama za Marekani, lakini haijawa wazi iwapo yuko miongoni mwa wale ambao wamekataliwa.

Waendesha mashitaka wa kijeshi wa Libya walikuwa wameiomba tume ya uchaguzi kuzuwia mchakato wa makaratasi ya kugombea ya Bw Gaddafi na Bw Haftar hadi watakapojibu maswali juu ya shutuma dhidi yao.

Watu sitini waliwasilisha maombi ya kugombea urais wa Libya kufikia Jumatatu.

Mwanaharakati wa haki za wanawake Leila Ben Khalifa, 46, ni mwanamke pekee anayegombe kiti hicho.