Waziri mkuu wa zamani wa Lesotho ashtakiwa kwa kumuua mkewe

Muhtasari
  • Bw Thabane alijiuzulu Mei 2020 kufuatia shinikizo la miezi kadhaa baada ya kutajwa kama mshukiwa
Image: BBC

Waziri Mkuu wa zamani wa Lesotho Thomas Thabane ameshtakiwa kwa mauaji ya mke wake Lipolelo Thabane mwaka 2017.

Mkewe wa sasa, Maesaiah, alishtakiwa kwa uhalifu kama huo mwaka jana.

Alikuwa akiishi na Bw Thabane wakati wa mauaji hayo na wanatuhumiwa kuajiri watu waliotekeleza shambulizi hilo. Wote wawili wamekana kuhusika.

Bw Thabane alijiuzulu Mei 2020 kufuatia shinikizo la miezi kadhaa baada ya kutajwa kama mshukiwa.

Kesi hiyo imewashangaza wengi na kusababisha misukosuko ya kisiasa katika ufalme huo mdogo usio na bahari ambao umezungukwa kabisa na Afrika Kusini.

Maesaiah Thabane aliandamana na waziri mkuu huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 82 hadi mahakamani. Alishtakiwa mwaka jana na kisha kuachiliwa kwa dhamana.

Mashtaka hayo yalisomwa katika ukumbi wa Mahakama Kuu katika mji mkuu wa Maseru, badala ya chumba cha mahakama kuu, jambo ambalo ni la kawaida, shirika la habari la AFP linaripoti.

Watu wenye silaha walimpiga risasi na kumuua Lipolelo Thabane tarehe 14 Juni 2017 - siku mbili kabla ya Bw Thabane kuapishwa kama waziri mkuu.

Alipokuwa akirudi nyumbani, aliviziwa, akapigwa risasi mara kadhaa akiwa karibu na akafa kando ya barabara. Alikuwa na umri wa miaka 58.

Wakati huo, Lipolelo alikuwa katikati ya kupata talaka kutoka kwa Bw Thabane na alikuwa akiishi kando na mumewe tangu 2012.

Alikuwa amehama kuanza kuishi na Maesaiah kwa muda kati ya 2012 na 2017. Walioana miezi miwili baada ya kifo cha Lipolelo.