Ethiopia yatwaa tena mji wa urithi wa dunia-Serikali

Mzozo wa Ethiopia wa Tigray: Lalibela yachukuliwa tena - serikali

Muhtasari

• Huu ni ushindi wa hivi punde zaidi kudaiwa na serikali tangu Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwenda mstari wa mbele wiki iliyopita kuongoza vita.

• Lalibela, maarufu kwa makanisa yake yaliyochongwa mwamba, ilitekwa na waasi mwezi Agosti.

• Miji mingine iliyochukuliwa tena kutoka kwa waasi ni pamoja na Shewa Robit, yapata kilomita 220 kutoka Addis Ababa, serikali ilisema.

Image: GETTY IMAGES

Wanajeshi wa Ethiopia wameuteka tena mji wa kihistoria wa Lalibela kutoka kwa waasi wa Tigraya serikali imesema.

Huu ni ushindi wa hivi punde zaidi kudaiwa na serikali tangu Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwenda mstari wa mbele wiki iliyopita kuongoza vita.

Chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) kilisema kimefanya "kujiondoa kwa kimkakati" kutoka kwa baadhi ya maeneo.

Lalibela, maarufu kwa makanisa yake yaliyochongwa mwamba, ilitekwa na waasi mwezi Agosti.

Ni eneo la urithi wa dunia la Unesco katika eneo la Amhara nchini Ethiopia, na lilikuwa kivutio maarufu cha watalii kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka nchini Ethiopia mwaka jana.

Mgogoro huo ulianza katika eneo la kaskazini la Tigray, na baadaye ulikumba maeneo mengine ya Ethiopia wakati TPLF ilipoanzisha mashambulizi kufika Addis Ababa kusini na mpaka na Djibouti upande wa mashariki, ambayo ni muhimu kwa ajili ya kupata mahitaji kwa Ethiopia isiyo na bandari.

Hofu ya waasi kwenda Addis Ababa ilisababisha nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, kuwataka raia wao kuondoka Ethiopia mwezi uliopita.

Mapema siku ya Jumatano, msemaji wa serikali Legesse Tulu alinukuliwa na vyombo vya habari vya serikali akisema wanajeshi pia wana uhakika wa kuutwaa tena mji wa kimkakati wa Dessie "katika muda mfupi".

TPLF iliuteka mji wa Dessie mwezi uliopita, katika kile kilichoonekana kuwa pigo kubwa kwa serikali kwani jiji hilo linaelekea Addis Ababa na pia mpaka na Djibouti.

Miji mingine iliyochukuliwa tena kutoka kwa waasi ni pamoja na Shewa Robit, yapata kilomita 220 kutoka Addis Ababa, serikali ilisema.

Televisheni yenye uhusiano na serikali ilirusha kanda za Bw Abiy siku ya Jumanne akiwa amevalia sare za kijeshi, akitazama akikagua eneo la vita kwa darubini.

"Adui ameshindwa. Kazi yetu iliyobaki ni kuwashinda adui na kuwaangamiza," aliwaambia askari walioketi chini ya miti.

Image: ETHIOPIAN PRIME MINISTER'S OFFICE

Wiki iliyopita, kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael aliandikia Umoja wa Mataifa, akielezea wasiwasi kuhusu mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya raia.

Ethiopia ilikuwa imepokea ndege zisizo na rubani za China, pamoja na silaha kutoka Iran, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bw Debretsion alisema.

Hakujawa na majibu yoyote kwa madai yake.

Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi kwa sasa yuko ziarani nchini Ethiopia. Anatarajiwa kukutana na Naibu Waziri Mkuu Demeke Mekonnen, ambaye amechukua mamlaka ya uendeshaji wa kila siku wa serikali huku Bw Abiy akiwa kwenye uwanja wa vita.

China ilikuwa imepinga "Kuingilia" kwa nchi za kigeni kwa masuala ya Ethiopia huku serikali ya Bw Abiy ikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kutokana na ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakati huo huo, serikali ya Ethiopia imeishutumu Twitter kwa kulenga akaunti ambazo zinawakosoa waasi.

Twitter imesema inasalia "kutofungamana na utambulisho wa kisiasa na itikadi".

Mwezi uliopita, Twitter iliondoa kwa muda utendakazi wake nchini Ethiopia, ikitaja ''tishio lililo karibu la madhara ya kimwili''.

Facebook iliondoa chapisho kutoka kwa Bw Abiy, ikisema kuwa linakiuka sera zake dhidi ya kuchochea ghasia.