Moto mkubwa wateketeza jengo la Bunge la kitaifa la Afrika Kusini

Muhtasari

•Maofisa wanasema moto huo ulianzia kwenye ofisi za ghorofa ya tatu na kuenea haraka hadi kwenye Bunge la Kitaifa

Image: REUTERS

Moto mkubwa umewaka katika jengo la Bunge katika jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini.

Picha za videoambazo zimesambazwa zinaonyesha moshi mwingi mweusi  ukijaa angani, huku miali mikubwa ya moto ikitoka kwenye paa la jengo hilo.

Makumi ya wazima moto wameonekana wakipambana na moto huo; bado haijafahamika chanzo cha moto huo.

Tukio hilo linakuja saa chache baada ya mazishi ya Askofu Mkuu Desmond Tutu katika Kanisa Kuu la St George, karibu na bunge.

Maofisa wanasema moto huo ulianzia kwenye ofisi za ghorofa ya tatu na kuenea haraka hadi kwenye Bunge la Kitaifa (baraza kuu la bunge), anaripoti mwandishi wa BBC Nomsa Maseko mjini Cape Town.

Hakuna watu waliojeruhiwa walioripotiwa na hakuna dalili ya kile kilichosababisha moto huo, mwandishi wetu anaongeza.

Maafisa wa kikosi cha zimamoto na uokoaji walisema inaweza kuchukua saa nyingine nne kuzima moto huo kabisa kwa sababu ya mazulia na sakafu ya mbao iko katika jengo hilo.

Waziri wa miundombinu , Patricia de Lille, awali alisema moto katika Baraza la Mikoa (baraza la juu) umezuiwa, lakini bado unaendelea kuwaka Bungeni.

Mjumbe wa kamati ya usalama Cape Town , JP Smith, aliwaambia waandishi wa habari kuwa paa lilikuwa limeporomoka kwa kiasi na kwamba kengele ya kutambua moto haikulia wakati moto huo ulipoanza kuwaka.

"Paa la jengo limeporomoka upande mmoja na moto umeenea hadi kwa mkutano mpya, kulingana na maafisa.

"Wamegundua nyufa kubwa kwenye ukuta, jambo ambalo linatia wasiwasi.

"Wazima moto wanaripoti kwamba walikuwa kwenye eneo la tukio kwa muda kabla ya mfumo wa kutambua moto kuanza na kisha kutoa tahadhari. Kwa hivyo inaonekana kwamba mfumo huo ulichelewa kwa kiasi fulani."

Hakuna mikutano inayoendelea Bungeni kwa sasa kwa sababu ya likizo.

Image: REUTERS

Jengo la Bunge huko Cape Town lina sehemu tatu, na kongwe zaidi ya 1884. Sehemu mpya zaidi zilizojengwa katika miaka ya 1920 na 1980 la Bunge la Kitaifa.

Mwaka jana, moto uliteketeza sehemu ya maktaba ya Chuo Kikuu cha Cape Town, ambayo ilikuwa na mkusanyiko wa kipekee wa kumbukumbu za Kiafrika.