Miili ya watu 44 yapatikana kwenye vifusi huku mapigano yakiendelea Ukraine

Muhtasari

• Waokoaji wameweza tu kulifikia jengo hilo, afisa mmoja wa eneo hilo alisema.

• Kuna hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi, kwani jengo lingine katika barabara hiyo hiyo pia lililengwa.

• Urusi ilitwaa udhibiti wa mji wa Izyum tarehe 1 Aprili na wanajeshi wameuteka mji huo tangu wakati huo.

Meya wa jiji hilo amethibitisha kuwa miili ya raia 44 ilitolewa kutoka kwenye vifusi Picha: MAKSIM STRELNIK/BBC
Meya wa jiji hilo amethibitisha kuwa miili ya raia 44 ilitolewa kutoka kwenye vifusi Picha: MAKSIM STRELNIK/BBC

Miili ya raia 44 imepatikana kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka katika mji wa Izyum nchini Ukraine huku vita vya kuwania udhibiti wa eneo hilo vikiendelea.

Jengo hilo la ghorofa tano liliporomoka mwezi wa Machi huku wakazi wakijificha kwenye vyumba vya chini kutokana na kushambuliwa kwa makombora na Urusi.

Lakini waokoaji wameweza tu kulifikia jengo hilo, afisa mmoja wa eneo hilo aliambia BBC.

Na kuna hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi, kwani jengo lingine katika barabara hiyo hiyo pia lililengwa.

"Tunajua pia kulikuwa na watu mle ndani. Kazi ya utafutaji inaendelea na nadhani tutajua idadi zaidi ya waathiriwa hivi karibuni," meya wa Izyum Valeriy Marchenko aliambia BBC.

Urusi ilitwaa udhibiti wa mji wa Izyum tarehe 1 Aprili na wanajeshi wameuteka mji huo tangu wakati huo.

Hakuna vifaa maalum vya kufukua kifusi na kila kitu kinafanywa kwa mikono. Wale wanaofanya kazi hiyo wanaweza tu kufanya hivyo wakati makombora yanaposimamishwa, kwa mujibu wa gavana wa mji wa Kharkiv Oleh Synyehubov.

Izyum, inayojulikana kama lango la kuelekea Donbas, ni sehemu ya eneo la zamani la Ukraine linalozalisha makaa ya mawe na chuma na mji muhimu kwa wanajeshi wa Urusi.