Salvador Ramos: Mfahamu kijana aliyeshambulia shule ya msingi Marekani na kuua watoto 19 na walimu wawili

Muhtasari

•Kijana huyo alitambuliwa kama Salvador Ramos, raia wa Marekani na mkazi wa mji wa Texas wenye wakazi 15,000 ulioko takriban kilomita 135 kutoka San Antonio.

•Sababu ya uhalifu huo bado haijafahamika, lakini polisi wanaripoti kwamba kila kitu kinaonekana kuashiria kwamba Ramos alitekeleza tukio hilo peke yake.

•Kabla ya kuondoka nyumbani, mhusika pia alimpiga risasi usoni bibi yake ambaye alipelekwa hospitalini akiwa katika hali mbaya.

Image: PLICIA DE TEXAS

Takriban watoto 19 na walimu wawili walifariki Jumanne hii katika shule iliyopo mji wa Uvalde, jimbo la Texas, baada ya mvulana wa miaka 18 kuingia akiwa na silaha na kuanza kufyatua risasi.

Kijana huyo alitambuliwa kama Salvador Ramos, raia wa Marekani na mkazi wa mji huo wenye wakazi 15,000 ulioko takriban kilomita 135 kutoka San Antonio.

Gavana wa Texas Greg Abbot alisema Rasamos alifariki baada ya kukabiliana na polisi shuleni. Maafisa wawili walipigwa risasi, lakini Abbot alisema wako katika hali nzuri.

Waathirika walikuwa ni wanafunzi wa darasa la 2, 3 na 4 wenye umri wa kati ya miaka 7 na 10. Walimu wawili pia walifariki kwa kupigwa risasi katika shule hiyo ya wanafunzi wapatao 500, wengi wao wakiwa na asili ya Amerika Kusini.

Sababu ya uhalifu huo bado haijafahamika, lakini polisi wanaripoti kwamba kila kitu kinaonekana kuashiria kwamba Ramos alitekeleza tukio hilo peke yake.

Kijana huyo alikuwa akiendesha gari la kubebea mizigo lililoanguka kwenye mtaro mita chache kutoka Shule ya Msingi ya Robb, ambapo aliingia na kuanza kufyatua risasi darasani.

Wakala wa Doria wa Mpaka wa Marekani ambaye alikuwa karibu wakati wa tukio hilo la ufyatuaji risasi lilipoanza aliingia shuleni na kumpiga risasi na kumuua kijana huyo mwenye bunduki, ambaye alikuwa nyuma ya kizuizi, shirika la habari la Associated Press liliripoti.

Image: REUTERS

Bunduki mbili kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa ya kutimiza miaka 18

Mshambuliaji huyo, akiwa amevalia fulana ya kuzuia risasi, alitoka kwenye gari lililoanguka akiwa amebeba bunduki na kisha kufyatua risasi kwenye jengo hilo, Sajenti Erick Estrada wa Idara ya Usalama wa Umma ya Texas aliiambia CNN.

Wachunguzi wanasema mhusika alikuwa amejihami kwa bunduki, bunduki aina ya AR-15 semi-automatic na bunduki yenye uwezo wa juu.

Mshambulizi huyo alikuwa amefikisha umri wa miaka 18 hivi karibuni na hakuwa na rekodi ya uhalifu, mamlaka ilithibitisha.

Ramos alinunua bunduki mbili aina ya AR na risasi 375 siku chache tu baada ya kutimiza miaka 18, kwa mujibu wa ripoti ya polisi wa jimbo iliyotumwa kwa Seneta Whitmire.

Moja ya bunduki hizo ilikutwa katika eneo la uhalifu, pamoja na rsasi saba za raundi 30, na nyingine ilipatikana kwenye gari lake lililoharibika nje ya shule, kulingana na ripoti.

Image: GETTY IMAGES

Kijana mwenye aibu aliyeonewa

Vyombo vya habari vya Marekani vimekuwa vikifichua maelezo kuhusu maisha na utu wa mshambuliaji huyo, akifafanuliwa na baadhi ya vijana wenzake kama kijana mpweke ambaye alipitia unyanyasaji na uonevu.

Mwanafunzi ambaye alikuwa rafiki wa Ramos akiwa darasa la nane aliambia Washington Post kwamba alikuwa kijana mwenye aibu ambaye mara kwa mara alikuwa akionewa na wanafunzi wenzake kwa sababu alikuwa na kigugumizi na kuchechemea, miongoni mwa sababu nyinginezo.

Aliripoti kwamba kijana huyo, ambaye alikuwa akicheza naye michezo ya video kama Fortnite na Call of Duty, alionyesha mabadiliko ya ajabu katika haiba yake na alianza kuwa na tabia zisizo za kawaida, kama vile kukata uso wake.

Pia alihakikishia kwamba rafiki yake alianza kuvaa nguo nyeusi kabisa na viatu vya kijeshi na kutohudhuria shuleni kwa muda mrefu, hivyo haikuonesha kama atahitimu masomo yake.

Kwa upande wake, jirani wa Ramos mwenye umri wa miaka 41 aliiambia CBS, mshirika wa BBC wa Marekani, kwamba Ramos "alikuwa na maisha magumu" na kwamba mama yake alikuwa mraibu wa dawa za kulevya na "hakuwahi kuonyesha upendo" kwake.

Pia alibainisha kuwa kuanzia umri wa miaka 14 au 15 tabia yake ilikuwa imebadilika, ilikuwa vigumu kufanya naye mazungumzo na alionekana kuwa "mtu aliyetengwa shuleni".

Kulingana na shuhuda, kijana huyo alikuwa na mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii na watu aliokutana nao mtandaoni.

Alimtambulisha msichana ambaye hakumfahamu binafsi katika chapisho la Instagram na picha ya bunduki hizo mbili kabla ya kutekeleza shambulio hilo.

Bibi yake

Kabla ya kuondoka nyumbani, mhusika pia alimpiga risasi usoni bibi yake ambaye alipelekwa hospitalini akiwa katika hali mbaya.

Taarifa zilionesha kuwa Ramos alikuwa mkazi wa Uvalde na alikuwa akisoma katika shule ya upili iliyo karibu.

Mshambuliaji huyo alikuwa na anwani ya nyanya yake kama anwani yake rasmi, kulingana na hati zilizopokelewa na taasisi za kushughulikia masuala ya pombe na sigara, Silaha za Moto na Vilipuzi.

Kulingana na Gavana Abbott, Ramos alichapisha machapisho matatu kwenye akaunti yake ya Facebook kabla ya kupigwa risasi.

Kwanza, kama dakika 30 awali, aliandika: "Nitampiga bibi yangu risasi."

Katika chapisho la pili alithibitisha kwamba alikuwa amefanya hivyo.

Katika chapisho la tatu, kama dakika 15 kabla ya shambulio lake kwenye shule kuanza, alitangaza kwamba angeenda kupiga risasi hule ya msingi.

Mama yake

'Hakuwa mtu wa vurugu'

Mama wa kijana huyu aliyeua watu 21 amezungumza kuhusu mwanae.

"Mwanangu hakuwa mtu wa fujo. Ninashangazwa na alichokifanya," Adriana Reyes aliliambia gazeti la Daily Mail kutoka hospitali ambako mama yake anapatiwa matibabu kutokana na jeraha la risasi usoni mwake (mshukiwa alimpiga risasi bibi yake kabla ya kushambulia shule, viongozi wa eneo wanasema).

Reyes alikanusha ripoti kwamba alikuwa na uhusiano mbaya na mtoto wake. "Nilikuwa na uhusiano mzuri naye. Alijitenga; hakuwa na marafiki wengi," aliambia gazeti hilo.

Reyes, 39, pia aliambia NBC News: "Nimesikitishwa sana na kila kitu. Mambo mengi yametokea, lakini kwa sasa sijisikii vizuri."

Juan Alvarez, mpenzi wa Reyes, aliiambia NBC mshambuliaji huyo alikuwa "mtu wa ajabu".

"Sijawahi kuelewana naye. Sikuwahi kujumuika naye. Hazungumzi na mtu yeyote," alisema Alvarez, 62.

"Unapojaribu kuongea naye hukaa tu na kuondoka."