Ukraine inapoteza wanajeshi 200 kwa siku - msaidizi wa Zelensky

Muhtasari

•Msaidizi mkuu wa rais wa Ukraine amesema kuwa kati ya wanajeshi 100 hadi 200 wa Ukraine wanauawa itani kila siku.

Image: BBC

Msaidizi mkuu wa rais wa Ukraine ameambia BBC kuwa kati ya wanajeshi 100 hadi 200 wa Ukraine wanauawa itani kila siku.

Mykhaylo Podolyak alisema Ukraine inahitaji mamia ya mifumo ya silaha za Magharibi ili kusawazisha uwanja na Urusi katika eneo la mashariki la Donbas.

Pia alisema Kyiv haiko tayari kuanza tena mazungumzo ya amani na Moscow. Wanajeshi wa Ukraine wanakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara huku majeshi ya Urusi yakijaribu kuchukua udhibiti wa Donbas nzima.

"Vikosi vya Urusi vimetumia kila aina ya silaha nzito dhidi yetu ikiwa ni pamoja na mifumo mingi ya kurusha roketi na anga," Bw Podolyak alisema.

Alirudia ombi la Ukraine la kutaka silaha zaidi kutoka kwa nchi za Magharibi, akisema kwamba "ukosefu kamili wa usawa" kati ya majeshi ya Urusi na Ukraine ndio sababu ya kiwango kikubwa cha vifo vya wanajeshi wa nchi hiyo.