Maafisa wa DR Congo waishutumu Rwanda kwa uvamizi

Muhtasari

•Waasi wa Kongo wa M23 waliuteka mji wa Bunagana siku ya Jumatatu baada ya kuwalazimisha baadhi ya wanajeshi wa serikali kukimbilia nchi jirani ya Uganda.

•Rwanda imerudia mara kadhaa kuuita mzozo wa mashariki mwa DR Congo "suala la ndani" na kukanusha kuwaunga mkono waasi wa M23.

Image: BBC

Maafisa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamelishutumu jeshi la Rwanda kwa kuvamia ardhi yake baada ya kudaiwa kuwasaidia waasi kuchukua Bunagana, mji wa mpakani katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Waasi wa Kongo wa M23 waliuteka mji huo siku ya Jumatatu baada ya kuwalazimisha baadhi ya wanajeshi wa serikali kukimbilia nchi jirani ya Uganda.

Mji huo wa kimkakati ni muhimu kwa biashara ya kuvuka mpaka kati ya DR Congo na Uganda.

Katika taarifa, mamlaka ya mkoa wa Kivu Kaskazini ilisema "jeshi la Rwanda liliamua kukiuka uadilifu wa eneo letu na kukalia mji wa Bunagana".

Walitaja kutekwa kwa mji huo "uvamizi wa DRC" na kuongeza kuwa jeshi "italinda taifa".

Rwanda imerudia mara kadhaa kuuita mzozo wa mashariki mwa DR Congo "suala la ndani" na kukanusha kuwaunga mkono waasi wa M23.

Jeshi lake halijatoa maoni yoyote kuhusu kutekwa kwa Bunagana, lakini katika taarifa yake siku ya Jumanne lilisema litahakikisha uadilifu wa ardhi ya Rwanda.

Mvutano kati ya majeshi hayo mawili umeongezeka baada ya kulaumiana kwa mashambulizi ya kuvuka mpaka mwishoni mwa juma.