Nyani amuua mtoto mchanga baada ya kumnyakua kutoka kwa mikono ya mamake

Muhtasari

•Mtoto aliumia kichwa na shingo baada ya  kuvamiwa na kundi la nyani wakati alipokuwa akinyonya nje ya nyumba yao.

•Baada ya nyani huyo kuzidiwa, alimtupa mtoto huyo chini akiwa tayari amejeruhiwa kichwani na shingoni.

Image: BBC

Mtoto mmoja Magharibi mwa Tanzania, amefariki dunia baada ya kuumia kichwa na shingo kwenye tukio la kushangaza la kuvamiwa na kundi la nyani wakati alipokuwa akinyonya nje ya nyumba yao.

Katika tukio hilo lililotokea juma lililopita (Juni 18), kundi la nyani kutoka hifadhi ya Gombe inayopakana na Kijiji cha Mwamgongo, wilayani Kigoma walimvamia, Shayima Said, mama na mkazi wa eneo hilo na kuondoka na mtoto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, James Manyama alithibitishia BBC kutokea kwa tukio hilo mnamo Juni 18 na kueleza kuwa baada ya tukio hilo mwanamke huyo alipiga kelele kuomba msaada na ndipo majirani zake walipojitokeza kumdhibiti nyani aliyekuwa amebeba mtoto huyo.

Hata hivyo alisema kuwa baada ya nyani huyo kuzidiwa, alimtupa mtoto huyo chini akiwa tayari amejeruhiwa kichwani na shingoni.

"Wananchi walifanikiwa kulikimbiza kundi hilo la nyani lililomvamia mwanamke huyo wakati akimnyonyesha wanaye, na kufanikiwa kumpata mtoto akiwa amejeruhiwa lakini baada ya kufikishwa katika kituo cha afya cha Mwamgongo alifariki dunia,"amesema Kamanda Manyama.