Nigeria yapiga marufuku digrii za Ukraine

Muhtasari
  • Mamia ya wanafunzi wa Nigeria walihamishwa kutoka Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi

Katika tangazo lililozua mshtuko, Baraza la Matibabu na Meno la Nigeria limesema halitatambua shahada kutoka vyuo vikuu vya Ukraine zilizopatikana tangu kuanza kwa vita vya nchi hiyo na Urusi.

Mdhibiti wa huduma za kitaalamu za afya nchini Nigeria pia hatakubali programu za matibabu na meno zinazotolewa mtandaoni.

Tangazo hili linafuatia kubadilishwa kutoka kozi za kuonana ana kwa ana hadi kozi za mtandaoni kwa wanafunzi wengi waliokuwa wakisoma nchini Ukraine ambao bado hawajakamilisha programu zao.

Baadhi ya wanafunzi hao waliozungumza na BBC wanasema ni pigo kubwa kwa masomo na taaluma zao, haswa kwa wale ambao walikuwa wametumia zaidi ya miaka mitano kusoma na wamebakiza miezi michache tu kuhitimu.

Wanaita sera hiyo kuwa ya kibaguzi, wakisema kwamba wanafunzi waliosoma kwa njia ya mtandao wakati wa janga la corona waliruhusiwa kuhitimu na kufanya mazoezi.

Wanafunzi pia wameikosoa serikali kwa kushindwa kuweka vyuo vikuu vya Nigeria wazi huku kukiwa na migomo ya hivi karibunii ya wahadhiri na kuwalazimisha kusoma mahali pengine.

Mamia ya wanafunzi wa Nigeria walihamishwa kutoka Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi.

Baraza la Madaktari na Meno, ambalo hudhibiti madaktari, madaktari wa meno na waganga wa tiba mbadala nchini Nigeria hivi karibuni limekataa mafunzo ya mtandaoni kutoka nchi nyingine, likisema kuwa hayafikii viwango vinavyokubalika.