(Video) Boko Haram wavamia gereza na kuwaachia huru wafungwa 600

Wanamgambo hao walisemekana kuwa 300 kwa idadi na walitekeleza uvamizi huo kwa saa 3 kabla ya jeshi la Nigeria kufika.

Muhtasari

• 600 hao walisemekana kuwa ni wanamgambo wenzao waliokuwa wamefungwa jela.

Taarifa kutoka nchini Nigeria zinaarifu kwamba wanamgambo wa kundi la Boko Haram juzi walivamia gereza moja nchini humo na kuwafungulia wafungwa zaidi ya 600.

Taarifa zinasema kwamba 600 hao wengi wao walikuwa ni wanamgambo wa kundi hilo hatari ambao walikuwa wamefungwa gerezani.

Haijulikani kamili idadi ya wanamgambo hao lakini baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa walikisiwa kuwa zaidi ya 300 na wakivamia gereza hilo lililoko takribani kilomita 35 kutoka jiji kuu la Abuja.

Tukio hilo la ajabu linaarifiwa kutokea siku mbili tu kabla ya watu wanaoaminika kuwa wanamgambo wa Boko Haram kuvamia msafara wa rais wa taifa hilo, Muhammadu Buhari.

Hii si mara ya kwanza kwa kundi hilo hatari kutekeleza vitendo vya kuitikiza dunia kwani mwaka wa 2014 Boko Haram walisemekana kulivamia shule moja ya wasichana na kuwateka nyara mamia ya watoto hao wa kike, ambao wengi wao walikuwa Wakristu.

Mamlaka kipindi hicho zilisema kwamba zaidi ya wasichana 276 waliripotiwa kutoweka baada ya uvamizi huo katika shule moja ya serikali.

Kitendo hicho kilishtumiwa kote ulimwenguni huku mataifa mbali mbali ya kigeni yakilitaka kundi hilo kuwaachia huru watoto wa shule na badala yake kupambana na wanajeshi wa kulinda amani ambao wamepelekwa katika sehemu tofauti tofauti zilizotajwa kushuhudia visa vya Boko Haram kutekeleza unyama kwa wananchi wasiokuwa na hatia, wengi wa waathiriwa wakiwa ni watu wa dini ya Kikristu.

Boko Haram ni kundi lenye itikadi kali la Kiislamu ambalo linaarifiwa wanachama wake wametapakaa katika sehemu kubwa ya kaskazini mwa taifa hilo wakipinga serikali ya Abuja huku wakidai kupatiwa uhuru wa kulianzisha taifa lao lenyewe kaskazini mwa Nigeria.