(Video) Miili 19 ya vijana waliopatikana wamefariki ndani ya klabu cha usiku yaagwa rasmi

Miili hiyo 19 ni miongoni mwa 21 ya vijana waliopatikana wamekufa ndani ya sehemu moja ya starehe.

Muhtasari

• Hafla ya mazishi ilifanyika katika eneo la East London nchini Afrika Kusini ambapo rais Ramaphosa alihudhuria.

• Kijana mdogo kabisa katika mkasa huo alikuwa binti wa miaka 13 tu!

Miili ya vijana 19 kati ya 21 iliyopatikana imetapakaa katika ukumbi mmoja wa burudani nchini Afrika kusini ilizikwa Jumatano katika hafla ya pamoja ya msiba huo ambayo rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alihudhuria.

Vijana hao 21 walipatikana wamefariki katika njia ya kutatanisha huku miili yao imetapakaa katika ukumbi wa starehe walikokuwa wamejumuika kusherehekea kumaliza mitihani ya kati kati ya muhula wiki moja iliyopita, tukio lililozua mjadala mkali sana mitandaoni huku baadhi wakidai huenda waliwekewa sumu kwenye vinywaji.

Vilio, huzuni, uchungu usiomithirika na majonzi yaligubika umati mkubwa uliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa vijana hao.

Tukio hilo lilitikisa taifa hilo huku ikiarifiwa kwamba mmoja wa walioaga dunia katika kundi hilo alikuwa binti wa miaka 13 tu aliyekuwa amwejumuika na wenziwe.

“Vijana wengi walio chini ya umri wa miaka 18 walikuwa wakinywa pombe ambayo ilikuwa imeuzwa kwao. Mtoto mdogo aliyekufa katika mkasa huu alikuwa na umri wa miaka 13 tu,” alisema rais Ramaphosa kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Licha ya miili hiyo kuagwa Jumatano, bado ripoti kamili ya upasuaji haijatoka ila wataalam wanahisi huenda vijana hao walipatana na umauti baada ya kuvuta kupitia hewa au kumeza.

Katika hafla hiyo, wengi walisihi rais Ramaphosa kuongeza umri wa mtu kuhalalishwa kunywa pombe kutoka 18 hadi 21.

Rais Ramaphosa kupitia msururu wa jumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter aliwaomboleza makinda hao ambao miili yao ilikuwa imewekwa kwenye majeneza mbele ya umati wa zaidi ya waombolezaji elfu 3.

“Hakuna maneno ambayo yanaweza kuleta faraja kwa wakati huu, lakini uchungu wanu na upunguzwe. Mioyo yenu na itulie; machozi yenu yafutwe. Tuko pamoja nanyi. Tunaomboleza pamoja nanyi. Na mnaweza kuwa na uhakika kwamba kama serikali, tutachukua hatua,” rais Ramaphosa aliomboleza.

Hii haikuwa mara ya kwanza ambapo watu wanapatana na mauit ya kutatanisha katika kumbi za starehe za usiku nchini humo kwani mwaka 2015, wanadada 8 pia walipatikana wamefariki kwa njia za kutatanisha, kando na kisa kingine kilichotokea mwaka 2000 ambapo pia watoto 13 walifariki na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika klabu moja cha usiku jijini Durban nchini humo.