Afrika Kusini: Watu 15 wamepigwa risasi katika baa Soweto

Watu kadhaa zaidi wako katika hali mbaya hospitalini.

Muhtasari

•Polisi walisema watu wenye silaha waliingia kwenye kilabu hicho asubuhi ya Jumapili na kuanza kufyatulia risasi ovyo kundi la vijana.

•Watu hao wenye silaha walikuwa wamejihami kwa bunduki na bastola za 9mm walipoingia kwenye baa hiyo.

Image: BBC

Takriban watu 15 wameuawa kwa kupigwa risasi katika baa moja katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini, polisi wamesema.

Polisi walisema watu wenye silaha waliingia kwenye kilabu hicho asubuhi ya Jumapili na kuanza kufyatulia risasi ovyo kundi la vijana.

Kisha wakatoroka eneo hilo kwa basi dogo jeupe.

Hakuna sababu ya shambulio hilo ambayo imebainishwa, polisi walisema.

Watu kadhaa zaidi wako katika hali mbaya hospitalini, mwandishi wa BBC Nomsa Maseko anaripoti.

Waathiriwa wanaaminika kuwa na umri wa kati ya miaka 19 na 35.

Jamaa za waathiriwa wamekuwa wakiomboleza nje ya baa hiyo
Jamaa za waathiriwa wamekuwa wakiomboleza nje ya baa hiyo
Image: bbc

"Miili ilikuwa juu ya kila mmoja huku damu zikiwa zimetapakaa. Tulikuwa tunawatafuta wapendwa wetu, ikabidi turuke miili kuwatafuta ndugu zetu," alisema mkazi wa eneo hilo Ntombikayise Meji.

Jamaa za waathiriwa wamekuwa wakiomboleza nje ya baa hiyoImage caption: Jamaa za waathiriwa wamekuwa wakiomboleza nje ya baa hiyo

Mkuu wa polisi wa jimbo la Gauteng, Lt-Jenerali Elias Mawela, aliiambia BBC kwamba ufyatuaji risasi huo unaonekana kuwa "shambulio la kinyama dhidi ya wateja wasio na hatia".

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi yake ilisema watu hao wenye silaha walikuwa wamejihami kwa bunduki na bastola za 9mm walipoingia kwenye baa hiyo.

Polisi wanawasaka washukiwa hao, ambao bado hawajafahamika majina yao, ilisema.

Thaban Moloi, kiongozi wa jamii huko Soweto, alikasirishwa na muda ambao iliwachukua polisi kufika katika eneo la tukio.

"Ni baya sana, nakwambia. Watu hawajui la kufanya. Ungekuwa huko ungeona wanawake na watoto wakilia," alisema.

Bw Moloi alisema shambulio hilo lilitokea saa 23:00 kwa saa za huko (21:00 GMT) siku ya Jumamosi lakini polisi hawakufika hadi saa 04:00 siku ya Jumapili.

"Ilichukua saa tano kwa wao kuja, jamani," alisema.