Watu watatu wafariki kutokana na ugonjwa usiojulikana Tanzania

Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa taarifa kuhusu ugonjwa wa ajabu uliokumba mkoa wa Lindi.

Muhtasari

• Taarifa zilisema kuwa ndani ya siku tatu walipokea wagonjwa wawili katika kituo hicho wakiwa na dalili za homa, kuvuja damu hususan puani, maumivu ya kichwa na mwili kuchoka sana.

Image: BBC

Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa taarifa kuhusu ugonjwa wa ajabu uliokumba mkoa wa Lindi.

Wizara hiyo imesema hadi kufikia tarehe 12 Julai kulikuwa na jumla ya wagonjwa 13, kati yao 3 wamefariki.

Wizara hiyo imesema kuwa tarehe 7 mwezi huu ilipokea taarifa kutoka kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Ruangwa kuwa kumekuwepo na ugonjwa usio wa kawaida kutoka kwenye kituo cha afya cha Mbekenyera.

Taarifa zilisema kuwa ndani ya siku tatu walipokea wagonjwa wawili katika kituo hicho wakiwa na dalili za homa, kuvuja damu hususan puani, maumivu ya kichwa na mwili kuchoka sana.

Hatua zilizochukuliwa

Wizara ya Afya imesema kwenye taarifa yake kuwa imeunda timu ya wataalam kutoka idara ya Magonjwa ya dharura na Majanga, Epidemiolojia, Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Utafiti (NIMR), Chuo kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Taasisi hizo zimeungana na timu ya Mkoa ikihusisha pia Idara ya Mifungo.

Idadi ya wagonjwa

Wagonjwa wawili waliokuwa wametengwa katika kituo cha Afya Mbekenyera, wamepona na kuruhisiwa kurudi majumbani mwao.

Wagonjwa wengine 5 wamejitenga katika makazi yao ya muda Wilayani Kilwa.

Mgonjwa mmoja ambaye amepona, anaendelea kufanya shughuli zake kijijini Mbekenyera.

Vile vile watu waliotangamana na wagonjwa hao (contacts) wamekuwa wakifuatiliwa afya zao kila siku na hadi sasa hakuna aliyeonesha dalili zozote zinazofanana na za wagonjwa hao.

Jitihada zinazofanyika kupambana na ugonjwa

Timu ya wataalamu inaendelea na ufuatiliaji. Sampuli za awali zilizopimwa katika maabara ya Taifa zimeonesha majibu hasi kwa ugonjwa wa Ebola, Marburg na Covid 19.

Wizara ya afya imesema kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi wa kiepidemiolojia na kitabibu pia wanasubiri matokeo ya vipimo zaidi vya maabara ya magonjwa ya Binadamu, Wanyama na Mkemia Mkuu wa Serikali.

Pia inaendelea;

  • Kutafuta watu wengine wenye dalili kama hizo ili kutambua mapema na kuwatenga ili kuzuia ugonjwa usisambae.
  • Kuwatambua watu wote waliotangamana (Contacts) na wagonjwa au wahisiwa au marehemu na kuwafuatilia kwa siku 21.
  • Wanatoa matibabu kwa wagonjwa waliobainika kuwa na dalili pia kuwashauri wajitenge wakati wakisubiria majibu ya vipimo vya maabara.
  • Serikali inatoa elimu kwa jamii kwa kutumia vyombo mabalimbali vya habari pia wamefanya maandalizi ya dawa , vifaa tiba na vifaa vya kujikinga na maambukizi kwa ajili ya kuwahudumia waathirika endapo watajitokeza tena.

Wizara ya Afya imesema taarifa ikikamilika Wizara itatoa taarifa kwa umma na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati ikiendelea kulifanyika kazi suala hili. Aidha imewataka wananchi waendelee kutumia vituo vya kutolea huduma za afya pale wanapojisikia kuumwa.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu hapo jana alikiri kuwepo kwa ugonjwa huo wakati akizungumza na viongozi wa dini katika Mkutano mkuu wa 20 wa Shirikisho la mabaraza ya maaskofu wa Kanisa Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA jijini Dar es Salaam.

''Nilikuwa nazungumza na Waziri Mkuu juzi, ametoka ziara kule mikoa ya kusini, Lindi ananiambia ameona kuna maradhi yameingia, wanadamu wanatokwa tu na damu za pua na wanadondoka'', alisema Rais Samia.

''Hatujui ni kitu gani, wanasayansi wataalamu wa afya wote wamehamia huko wanaangalia ni kitu gani'' alisema Rais Samia.

Rais Samia alikuwa akizungumza kwenye mkutano huo wa AMECEA, Shirikisho linaloundwa na nchi 8 ambazo ni Zambia, Malawi, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia, Eritrea na mwenyeji Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengine umejiegemeza kwenye masuala ya utunzaji wa mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu ya binadamu.