Joto kali laua watu 238 na kusababisha moto mkubwa Ulaya

Mamlaka ya Ureno inasema takriban watu 238 wamekufa kutokana na joto hilo katika wiki iliyopita.

Muhtasari

•Wataalamu wa zima moto wanaendelea kukabiliana na janga la moto katika nchi za Ureno, Hispania na Ufaransa.

•Moto unateketeza maeneo ya kusini-magharibi mwa mkoa wa Gironde nchini Ufaransa, ambapo zaidi ya watu 12,000 wamehamishwa.

Watu wengi wanalala katika maeneo ya fukwe kwa ajili ya kupooza miili yao kutokana na joto kali, Ulaya
Watu wengi wanalala katika maeneo ya fukwe kwa ajili ya kupooza miili yao kutokana na joto kali, Ulaya
Image: BBC

Maelfu ya wataalamu wa zima moto wanaendelea kukabiliana na janga la moto katika nchi za Ureno, Hispania na Ufaransa, huku wimbi la joto kali likionyesha kutokuwa na dalili ya kupunguza.

Kaskazini mwa Ureno, rubani alifariki wakati ndege yake ya kusaidia shughuli za zima moto ilipoanguka katika eneo la Foz Coa, karibu na mpaka wa Hispania. Mamlaka ya Ureno inasema takriban watu 238 wamekufa kutokana na joto hilo katika wiki iliyopita.

Moto unateketeza maeneo ya kusini-magharibi mwa mkoa wa Gironde nchini Ufaransa, ambapo zaidi ya watu 12,000 wamehamishwa.

Vipindi vya joto vimekuwa vikitokea mara kwa mara, kukileta wimbi kali zaidi la joto, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na shughuli za binadamu.

Kwa sasa joto duniani limeongezeka kwa takriban nyuzi joto 1.1C tangu enzi ya viwanda ianze na halijoto itaendelea kuongezeka kama serikali kote ulimwenguni hazitafanya juhudi za kupunguza kiwango cha uzalishaji wa kaboni.

Mamlaka ya hali ya hewa Ufaransa imetabiri viwango vya joto vya hadi nyuzi joto 41 katika sehemu za kusini mwa nchi siku ya leo Jumapili na rekodi mpya za joto zinatabiriwa kuendelea kesho Jumatatu.

Mkazi mmoja kusini-magharibi mwa Ufaransa alielezea moto mkubwa uliozuka msituni kama hisia "baada ya apocalyptic" - "Sijawahi kuona hii hapo awali," Karyn, anayeishi karibu na Teste-de-Buch, aliliambia shirika la habari la AFP.

Waziri wa Mambo ya Ndani Gerald Darmanin alisema moto hadi sasa umeteketeza hekta 10,000 (ekari 25,000) za ardhi na kusifu "ujasiri wa ajabu" wa wazima moto.

Maelezo ya picha,

Manon Jacquart alikuwa miongoni wa watu waliookolewa na kuondolewa Jumatano kwenye makazi yao kutokana na joto amekuwa akiishi kwenye eneo maalumu waliokohifadhiwa watu mbalimbali

"Kila kitu kilikwenda kwa haraka sana - moto pia, ulikuwa mkubwa, mkubwa, mkubwa," Manon Jacquart, 27, aliiambia BBC. Aliondolewa kwenye kambi anayofanya kazi mapema Jumatano asubuhi, na amekuwa akilala kwenye makazi karibu na La Teste-de-Buch, kwenye pwani ya magharibi ya Ufaransa.

"Nina wasiwasi tu, naogopa... ninajaribu kuwa na nguvu kadiri niwezavyo lakini siko sawa... nataka kusahau wiki hii," alisema.

Tangu Jumanne, joto limepanda hadi kufikia nyuzi joto 47 nchini Ureno na zaidi ya nyuzi joto 40 nchini Hispania, na kusababisha ukame na ukavu unaochochea moto. Watabiri wa hali ya hewa wa Ureno wanasema joto kali litaendelea kukuwa juu ya nyuzi joto 40 kabla ya kushuka wiki ijayo.

:Watu wakipoza miili yao kutokana na joto huko Madrid, Hispania
:Watu wakipoza miili yao kutokana na joto huko Madrid, Hispania
Image: BBC

Moto mkubwa mwingine umeteketeza kaskazini - mashariki mwa jiji la Porto, huko Ureno. Moto umeharibu hekta 30,000 (ekari 75,000) za ardhi mwaka huu - eneo kubwa zaidi tangu msimu wa joto wa 2017, wakati Ureno ilikumbwa na moto mbaya ambapo watu 100 walikufa.

Gemma Suarez, mkulima wa Hispania aliyehamishwa kutoka Casas de Miravete, alilia alipoiambia shirika la habari la Reuters: "Usiku ulioje. Hatujalala usiku kucha. "Mfanyakazi wa kijamii alikuja kuniona ili kwenda kumchukua mjomba wangu mzee. Tulilala huko Navalmoral lakini hatukulala kabisa. Sijawahi kuona moto mkubwa kama huu."

Kusini mwa Hispania watu wanaokwenda kujipumzisha kwenye ufukwe wa Torremolinos waliona moshi mwingi ukipanda milimani, ambapo ndege kadhaa zilikuwa zikikabili moto huo. Ashley Baker, Muingereza anayeishi Mijas, aliiambia BBC kwamba moto huo ulionekana kuwa wa kutisha zaidi siku ya Ijumaa, lakini tangu wakati huo upepo uliupeperusha kutoka eneo lake.

Ndege zimekuwa zikisaidia kuzima moto. Helikopta husafiri kwenda na kutoka pwani, kukusanya maji ya bahari ili kuzima moto.

"Kuna takriban nyumba 40 katika eneo letu, kila mtu alikuwa na wasiwasi na kusimama nje au kwenye balcony akiitazama," Bw Baker alisema. "Hata sasa hivi kuna moto kwenye mlima uliopo jirani. hatari."

Sehemu zingine za Bahari ya Mediterania zimeathiriwa pia. Nchini Italia, serikali imetangaza hali ya hatari katika Bonde la Po lililoharibiwa ambalo ni mto mrefu zaidi nchini humo.

Nchini Ugiriki, wazima moto wanakabiliana na moto katika eneo la Feriza, takriban kilomita 50 (maili 31) kusini-mashariki mwa Athens, na karibu na Rethymno, kwenye pwani ya kaskazini ya Krete.

Vijiji saba vimehamishwa karibu na Rethymno. Kaskazini mwa Morocco, vijiji kadhaa vililazimika kuhamishwa huku moto ukipita katika majimbo ya Larache, Ouezzane, Taza na Tetouan.

Kijiji kimoja kiliharibiwa kabisa katika eneo la Ksar El Kebir na angalau mtu mmoja alikufa kwa moto.