Japan: Polisi kuchukua hatua baada ya tumbili-mwitu kufanya ghasia

Katika wiki za hivi karibuni, watu 42 wameripotiwa kujeruhiwa katika jiji la Yamaguchi - ikiwa ni pamoja na watoto na wazee.

Muhtasari

• Juhudi za kuwakamata wanyama hao kwa mitego zilimalizika bila mafanikio na doria za polisi zilizotekelezwa tangu shambulio la kwanza mwanzoni mwa mwezi Julai zimeshindwa kuwazuia

Image: BBC

Polisi wa Japani wanageukia bunduki za kutuliza katika jaribio la kuzuia wimbi la mashambulizi ya tumbili-mwitu ambayo yamekuwa yakiwatia hofu wakazi.

Katika wiki za hivi karibuni, watu 42 wameripotiwa kujeruhiwa katika jiji la Yamaguchi - ikiwa ni pamoja na watoto na wazee.

Mashambulizi hayo yanalaumiwa aina ya tumbili wa zamani waliopo nchini Japan.

Hata hivyo, ingawa ni tukio la kawaida katika sehemu kubwa za nchi, matukio kama haya si ya kawaida.

‘’Ni nadra kuona mashambulizi mengi kama haya kwa muda mfupi,’’ afisa mmoja wa jiji alisema, akikataa kutajwa jina.

‘’Hapo awali ni watoto na wanawake pekee ndio walishambuliwa. Hivi karibuni wazee na wanaume watu wazima wamelengwa pia.’’

Juhudi za kuwakamata wanyama hao kwa mitego zilimalizika bila mafanikio na doria za polisi zilizotekelezwa tangu shambulio la kwanza mwanzoni mwa mwezi Julai zimeshindwa kuwazuia.

Mamlaka pia hazina uhakika kama mashambulio hayo ni ya tumbili mmoja au kadhaa.

Majeraha yamekuwa tofauti, huku vyombo vya habari vya ndani vikiripoti waathiriwa wamekwaruzwa miguuni na mikononi, hadi shingoni na matumboni.

Simulizi za mashambulizi zilizopo ni pamoja na msichana wa miaka minne aliyekwaruzwa wakati wa uvunjaji wa nyumba, huku tukio lingine likiwa la tumbili kuvunja darasa la shule ya chekechea.

Baadhi ya wakazi wameripoti uvamizi mara nyingi katika nyumba zao huku tumbili hao wakiwafikia kwa kutelezesha milango ya skrini au kuingia kupitia madirisha yalio wazi.

“Nilisikia kilio kikitoka kwenye orofa ya chini, kwa hiyo nikashuka haraka,” baba mmoja aliambia vyombo vya habari vya Japani.

‘’Kisha nikaona tumbili akimvizia mtoto wangu.’’