Kiongozi wa Al-Qaeda auawa katika shambulizi la ndege isiyo na rubani ya Marekani

Zahawiri aliuawa katika shambulio la ndege isiyo kuwa na rubani lililotekelezwa na CIA katika mji mkuu wa Kabul

Muhtasari

•Inaripotiwa kuwa Ayman al-Zawahiri aliuawa katika shambulio la ndege isiyo kuwa na rubani lililotekelezwa na CIA katika mji mkuu wa Kabul siku ya Jumapili.

•Zawahiri mara nyingi alijulikana kama mtu wa karibu wa Bin Laden na mwanaitikadi mkuu wa al-Qaeda.

Zawahiri alichukua uongozi wa al-Qaeda kufuatia mauaji ya Osama Bin Laden Mei 2011.
Zawahiri alichukua uongozi wa al-Qaeda kufuatia mauaji ya Osama Bin Laden Mei 2011.
Image: BBC

Operesheni ya kukabiliana na ugaidi nchini Afghanistan imemuua kiongozi wa kundi la al- Qaeda, Ayman al-Zawahiri, Rais Joe Biden amethibitisha.

Vinasema kwamba aliuawa katika shambulio la ndege isiyo kuwa na rubani lililotekelezwa na CIA katika mji mkuu wa Kabul siku ya Jumapili.

Hakuna habari zilizohuru kuthibitisha hilo kufikia sasa. Hatahivyo , Ikulu ya Whitehouse inasema kwamba rais Joe Biden atatoa maelezo ya kina kuhusu operesheni hiyo nchini Afghanistan katika saa chache zijazo.

Chombo cha habari cha CBC News kimesema kwamba vyanzo vitatu vimethibitisha mauaji hayo ya kiongozi huyo wa al-Qaeda. Chombho cha Habari cha New York Times, Washington Post na CNN vimenukuu vyanzo visivyojulikana vikimtambua muathiriwa.

Afisa mmoja mkuu amezungumza kuhusu operesheni iliofanikiwa dhidi ya malengo muhimu nchini Afghanistan.

 Operesheni hiyo ilifanyika wikendi iliopita na hakukuwa na raia waliojeruhiwa, maafisa hao walisema.

Wakati huohuo, msemaji wa Taliban aliripoti kwamba shambulizi la ndege ya marekani isio na rubani lilifanyika siku ya Jumapili katika eneo la makaazi ya watu mjini Kabul.

Alieleza kuwa ni ukiukaji wa wazi wa kanuni za kimataifa.

"Vitendo kama hivyo ni marudio ya uzoefu uliofeli wa miaka 20 iliyopita na ni kinyume na maslahi ya Marekani, Afghanistan na kanda," msemaji huyo aliongeza.

Zawahiri, daktari wa upasuaji wa macho ambaye alisaidia kupatikana kwa kundi la wanamgambo wa Kiislam la Egypt Islamic Jihad, alichukua uongozi wa al-Qaeda kufuatia kuuawa na vikosi vya Marekani kwa Bin Laden Mei 2011.

Kabla ya hapo, Zawahiri mara nyingi alijulikana kama mtu wa karibu wa Bin Laden na mwanaitikadi mkuu wa al-Qaeda.

Anaaminika na baadhi ya wataalam kuwa "mmoja ya watu waliobuni, kuratibu na kutekeleza mashambulizi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani..

Akiwa daktari wa Misri ambaye alifungwa miaka ya 1980 kwa kujihusisha na wanamgambo wa Kiislamu, aliondoka nchini baada ya kuachiliwa na kujihusisha na vuguvugu la kimataifa la wanajihadi.

Hatimaye aliishi Afghanistan na kuungana na tajiri wa Saudia, Osama Bin Laden. Kwa pamoja walitangaza vita dhidi ya Marekani na kuandaa mashambulizi ya Septemba 11, 2001.

Ilichukua muongo mmoja kwa Bin Laden kutafutwa na kuuawa na Marekani. Baada ya hapo, Zawahiri alichukua uongozi wa al-Qaeda, lakini akawa mtu wa mbali na wa pembeni, akitoa ujumbe mara kwa mara.

Iwapo kifo chake kitathibitishwa, Marekani itatangaza ushindi huo, hasa baada ya kujiondoa katika ghasia za Afghanistan mwaka jana, lakini Zawahiri alishikilia mamlaka kidogo huku makundi mapya na vuguvugu kama vile Dola la Kiislamu likizidi kuwa na ushawishi mkubwa. Kiongozi mpya wa al-Qaeda bila shaka ataibuka, lakini atakuwa na ushawishi mdogo hata kuliko mtangulizi wake.

Mauaji yake yaliyoripotiwa huko Kabul pia yanaashiria umuhimu wa kuendelea kwa Afghanistan - kumekuwa na wasiwasi kwamba makundi ya kigaidi yangeweza kupata nafasi zaidi ili kufanya kazi sasa na Taliban waliorejea katika udhibiti na kwamba taifa hilo lilitarajiwa kuwa maficho ya wapiganaji hao.

Lakini Marekani imeonyesha bado inaweza kushambulia kutoka mbali, hata ikiwa haipo tena katika ardhi ya nchi hiyo.