Mwili wa mwanajeshi aliyepotea miaka 38 iliyopita wapatikana kwenye barafu

Harbola alipotea mwaka 1984 wakati wa operesheni ya doria katika eneo la barafu la Siachen.

Muhtasari

•Miili 15 ilipatikana huku askari wengine watano hawakujuliana walipo wala miili yao kuonekana, akiwemo Chandrashekhar Harbola.

•Mkewe hakutaka kuolewa kwa kuwa aliamini yuko hai mahali, labda ametekwa au kuwekwa kizuizini na wapakistan, waliokuwa wakipambana nao vitani.

Image: BBC

Mama, baba atakuja lini nyumbani?" Mabinti wawili wa Shanti Devi walimuuliza swali hili kila siku kwa miaka mingi. Kila mara alikuwa akiwaambia kwamba baba yao yupo kazini na angerudi nyumbani hivi karibuni.

Miaka ilipita, lakini mazungumzo yao yalibaki vilevile. Baba yao, Chandrashekhar Harbola - askari wa jeshi la India - alipotea mwaka 1984 wakati wa operesheni ya doria katika eneo la barafu la Siachen.

Kikosi kilichokuwa na skari 20 kilinaswa katika maporomoko ya theluji katika kile kinachojulikana kama uwanja wa mapambano au vita uliojuu zaidi duniani (milimani), kwenye mpaka wa India na Pakistan.

Miili 15 ilipatikana huku askari wengine watano hawakujuliana walipo wala miili yao kuonekana, akiwemo Chandrashekhar Harbola.

Alipotangazwa kutoweka, binti yake mkubwa Kavita alikuwa na umri wa miaka minane, huku Babita akiwa na miaka minne.

Karibu miongo minne baadaye, hatimaye walipata habari kuhusu baba yao, lakini si aina waliyokuwa wakitarajia. Kwamba amefariki. Na muda wote huo mama yao, hakutaka kuolewa kwa kuwa aliamini mumewe yuko hai mahali, labda ametekwa au kuwekwa kizuizini na wapakistan, waliokuwa wakipambana nao vitani.

Mwili ulipatikanaje miaka 38 baadaye?

Kikosi cha jeshi kilikuwa katika doria ya kawaida wiki iliyopita na kuona eneo maalumu linalotumiwa na wanajeshi kujificha ama kuikinga na risasi ama bomu. Walipokaribia wakakuta mwili. Wakaona na namba ya kitambulisho cha jeshi na kikosi cha Harbola, iliyochorwa kwenye kipande cha chuma.

Walifikisha taarifa hizo makao makuu na baada ya ukaguzi wa kina wa kumbukumbu zao, walibaini kuwa mwili huo ulikuwa wa askari aliyepotea, Chandrashekhar Harbola.

"Tulipata taarifa hizi usiku wa Agosti 13', alisema mpwa wake na Harbola, Harish Chandra Harbola. Ulipatikana mwili mwingine katika eneo hilo, lakini haujatambulika ni wa nani mpaka sasa.

Matukio ya kuvunja moyo

Kavita, ambaye sasa ana umri wa miaka 46, na Babita, ambaye sasa ana umri wa miaka 42, walikuwa wakisubiri pamoja na mama yao wakati lori lililobeba mwili wa Harbola lilipofika.

Umati mkubwa wa ndugu, majirani na wananchi walikuwa wamekusanyika kumpa heshima zake. Tukio hilo lilikuwa likiambatana na nyimbo mbalimbali za huzuni ukiwemo unaosema Chandrashekhar Harbola hawezi kufa.

Kila mtu aliyekuwepo machozi yalimtoka. Na wengi wao hawakuamini kwamba mwili wake ulikuwa umepatikana. Sio kila siku ambapo mwili hupatikana baada ya miaka 38 na kuletwa nyumbani kwa heshima kamili ya kijeshi. Kwa familia yake, suala hili limefungwa. Lakini uchungu wa kukatishwa tamaa kwa matumaini utakaa kwa muda mrefu