'Mtu mpweke zaidi duniani' aaga dunia

Mwanaume huyo, ambaye jina lake halikujulikana, alikuwa ameishi peke yake kwa miaka 26.

Muhtasari

•Mwili wake ulipatikana tarehe 23 Agosti kwenye chandarua nje ya kibanda chake kilichojengwa kwa nyasi.

Mwaka 1998, mwanamume huyo alirekodiwa akikabiliana na mnyama pori
Image: BBC

Mtu wa mwisho aliyesalia wa kundi moja la asili nchini Brazil amefariki dunia, maafisa wanasema.

Mwanaume huyo, ambaye jina lake halikujulikana, alikuwa ameishi peke yake kwa miaka 26.

Alijulikana kwa jina la ‘’Mtu mpweke zaidi duniani’’ kwa sababu alichimba mashimo yenye kina kirefu, ambayo baadhi yake aliyatumia kunasa wanyama huku wengine wakionekana kujificha.

Mwili wake ulipatikana tarehe 23 Agosti kwenye chandarua nje ya kibanda chake kilichojengwa kwa nyasi.

Hakukuwa na dalili zozote za kuwa kulikuwa na vurugu.

Mtu huyo alikuwa wa mwisho kati ya kundi la wenyeji ambalo watu wa jamii yake wengine sita waliobaki waliuawa mwaka wa 1995. Kundi hilo liliishi katika eneo la wenyeji la Tanaru katika jimbo la Rondônia, ambalo linapakana na Bolivia.

Wengi wa kabila lake walidhaniwa kuuawa mapema kama miaka ya 1970 na wafugaji wanaotaka kupanua ardhi yao.

Mtu huyo anadhaniwa kuwa na umri wa miaka 60 na alikufa kwa sababu za asili.

Hakukuwa na dalili zozote za uvamizi katika eneo lake na hakuna chochote katika kibanda chake kilichotatizwa, maafisa walisema, lakini polisi bado watafanya uchunguzi wa maiti.

Chini ya katiba ya Brazil, watu wa kiasili wana haki ya ardhi yao ya kitamaduni, kwa hivyo wanaotaka kuinyakua wamejulikana kuwaua.

‘’Mtu huyo mpweke’’ alikuwa akifuatiliwa kwa usalama wake mwenyewe na mawakala kutoka Shirika la Masuala ya Wenyeji la Brazili tangu mwaka 1996.

Mnamo 2018, mtu mmoja aliweza kumrekodi wakati anakabiliana na mnyama pori.

Katika picha hiyo, anaonekana akichungulia kwenye mti akiwa na kitu kinachofanana na shoka.

Na tangu wakati huo hakukuwa na taarifa zozote za kuonekana kwake lakini maafisa walitembelea eneo alilokuwa akiishi lenye mashimo makubwa aliyochimba.

Ushahidi uliopatikana kwenye eneo alilokuwa anaishi unaonesha alipanda mahindi na matunda kama vile papai na ndizi.

Kuna takribani makabila 240 ya kiasili nchini Brazili, huku mengi yakiwa kwenye tishio la kutoweka kutokana na wachimbaji haramu, wakataji miti na wakulima kuvamia eneo lao.