Zifahamu nchi 5 zenye unafuu zaidi wa tozo na kodi duniani

Nchi zinazo toza kodi za chini mno ni Bahamas, Brunei, Panama, Bermuda na UAE

Muhtasari

• Nchi zinatambulisha kodi na tozo mbalimbali za msingi ilikufikia malengo yake ya utoaji wa huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo.

 

Image: BBC

Sio rahisi duniani kukuta nchi haitozi tozo au kodi kabisa, kwa sababu mapato yatokanayo na tozo na kodi yanasaidi kufadhili bajeti ya nchi inayoshughulikia huduma na shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo miradi.

Hoja inakuja ni tozo ama kodi ngapi zinawekwa, unaziweka maeneo gani na viwango gani vya gharama za hizo kodi ama tozo unakata?

Pengine maswali haya ndiyo yanaleta mjadala mkubwa kwa nchi hasa zenye uchumi mdogo kama za kiafrika. Nchi hizi ni lazima zitumie kodi na tozo kupata mapato ya kujiendesha na kuhudumia wananchi wake kutokana na viwango vya uchumi ilivyonavyo.

Kwa mantiki hiyo, nchi zinatambulisha kodi na tozo mbalimbali za msingi ilikufikia malengo yake ya utoaji wa huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo.

Kodi kwenye mapato kwa wafanyabiashara binafsi (income tax), kodi ya mapato kwa makampuni (corporate tax), kodi ya mapato kwa wafanyakazi (mfano PAYEE), michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii (Social security), Kodi ya majengo (property tax), kodi ya ardhi, kodi na ushuru wa kusafirisha na kuingiza bidhaa nchini, kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kodi ya faida ya mtaji (capital gains tax) na kodi nyingine nyingi.

Zipo kodi, ushuru na tozo lukuki tu kulingana na utafiti, maoni na rasilimali za nchi husika huwekwa kwa lengo hilo hilo la kukusanya mapato.

Image: BBC

Kwa sasa nchini Tanzania kumekuwa na mijadala mikubwa inayouhusu tozo na kodi. Mijadala inayozunguka kwenye tozo katika miamala ya simu, benki, visimbuzi, kwenye mita za umeme-Lipa Umeme Kadiri Unavyotumia (LUKU), tozo kwenye mafuta ya diseli, taa na petroli na pia kadi za simu.

Tozo hizi zinagusa mapato binafsi ya mtu, ambayo pengine yashakatwa kodi zingine (personal income tax).

Baadhi wakilalamika kukatwa tozo ama kodi mara mbili kwa mapato yale yale na kwa viwango vinavyoonekana kama mzigo kwa mwananchi.

Serikali ya nchi hiyo kupitia waziri wake wa fedha, Mwigulu Nchemba imejitokeza na kusema imepokea mijadala na malalamiko kuhusu tozo na sasa inakwenda kufanyia kazi.

Sasa zipo nchi ambazo mijadala ya aina hii haisikiki sana, si sababu haitozwi kodi ama tozo kabisa, zinatoza ila zaidi kwenye mapato ya faida ya biashara, kwa viwango vya chini na zingine hazigusi mapato binafsi ya watu wake.

Bahamas

Image: BBC

Bahamas ni moja ya visiwa vya kuvutia zaidi linapokuja suala la kuishi na kufanya biashara. Ni miongoni mwa nchi zenye unafuu zaidi wa kodi na tozo kwenye mapato binafsi ya nchi.

Ukiacha kuwa na fukwe za kuvutia Bahamas ni taifa lisilo na kodi ya mapato binafsi lakini pia kwenye magawio na kwenye mitaji.

Mfanyakazi anatozwa 3.9% kwa ajili ya michango kwenye mfuko wa hifadhi ya jamiii ambayo hata hiyo ilionekana kubwa na kupendekezwa kufikia 3.4% huku ikitoza asilimia 12% ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa na huduma zote kasoro vyakula na baadhi ya huduma za afya.

Brunei

Image: BBC

Nchi hii inatajwa kuwa taifa pekee kusini Mashariki mwa bara la Asia ambalo halina kodi ya mapato, kwa mujibu wa utafiti wa mtandao maarufu wa offshorecitizen.net.

Ukiacha kodi kwenye biashara zinazoleta faida, nchi hii inatoza mapato binafsi asilimia 5% kama michango ya kijamii kwenye mfuko wa taifa.

Hivyo kuwa miongoni mwa nchi chache duniani zenye haueni ya kodi kwa mapao binafsi ya mtu.

Panama

Image: BBC

Panama nayo ina afueni kubwa ya kodi ya mapato ya mtu binafsi ambapo kama mapato yako kwa mwaka yako chini ya dola $11,000 kama shilingi  Shilingi 1,254 za Kenya basi hautozwi kodi. 

Lakini ukiwa na kipato cha kuanzia dola $11,000 na $50,000 utalipa asilimia 15% na kama kipato chako kimezidi sola $50,000 utakatwa 25%.

Kwa watu wenye kipato cha chini wana afueni kubwa zaidi kuliko wenye kipato cha juu ukiwa katika nchi hii ya Panama. Ingawa wanaguswa na kodi ya wanandoa ama wenza ya dola $800 kama inavyobainishwa na mtandao wa shirika la kimataifa la International relocation firm.

Bermuda

Image: BBC

Kwa mujibu wa Mtandao wa serikali wa Bermuda (www.gov.bm), mtu binafsi hapaswi kulipa kodi ya mapato, ila Serikali imeweka tozo inayoitwa Payroll Tax yaani tozo ama kodi ya malipo ya mshahara.

Kupitia kodi hii kila mfanyakazi anakatwa asilimi 6 ya mshahara wake unaokwenda serikalini. Imeweka tozo hii kama kuongeza tu uwajibikaji wa wananchi wake kwenye kuchangia shughuli na huduma za maendeleo.

UAE

Image: BBC

Ni nchi inayofahamika kwa ukuaji wake wa kasi wa maendeleo. Mafuta yanasaidia sana kujenga uchumi wa taifa hili la kiarabu. Sekta ya binafsi katika taifa hili imekuwa imara zaidi ikivutia wawekezaji wengi wa ndani na nje. Yote ni kwa sababu ya mfumo wake wa masuala ya kodi kuwa rafiki kwa wazawa na wageni.

Ilitambulisha kodi ya VAT ya asilimia 5% miaka ya hivi karibuni ambayo bado ni nafuu ukilinganisha na mataifa mengi duniani.