Mwanamke amuua mtoto wa 'side-chick' wa mume wake, akamatwa akimfukia

Inasemekana mtuhumiwa alikuwa ametengana na mumewe kwa muda mrefu kabla ya kumpata mtoto huyo wa miaka 6 na kuamua kumuua.

Muhtasari

• Mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina Happiness Mkolwe mwenye umri wa miaka 27 alikutwa akichimba kaburi ili kumzika mtoto.

Crime scene
Crime scene
Image: MAKTABA

Inasikitisha sana kwamba mauaji ya kikatili katika siku za hivi karibuni ndio habari ya mjini, haswa katika mataifa mengi ya Kiafrika, mengine yakitokana na msongo wa mawazo, mizozo ya kila aina na wivu wa kimapenzi

Nchini Tanzania katika mkoa wa Njombe, polisi walimkamata mwanamke mmoja aliyesemekana kumuua mtoto wa mwanamke aliyesemekana kuzaa na mumewe mtuhumiwa – mtoto wa mchepuko.

Mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina Happiness Mkolwe mwenye umri wa miaka 27 alikutwa akichimba kaburi ili kumzika mtoto huyo wa kiume mwenye miaka 6, na kiini cha kumuua ilisemekana ni kwa sababu aligundua mtoto huyo alizaliwa na mumewe nje ya ndoa.

Shirika la Habari la The Guardian nchini Tanzania kupitia ukurasa wake wa Twitter liliripoti kwamba Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issah alisema Mwanamke huyo alimchukua Mtoto na kumsababishia kifo na kumfukia kwenye takataka za mbao kabla ya kushtukiwa alipokuwa akichimba shimo kwa ajili ya kumfukia.

“Alivyomsababishia kifo alimvua nguo na kumpeleka kwenye takataka za mbao alikochimba na kumfukia kwasababu ni laini lakini haikutosha aliamua kuchimba kaburi pembeni ili amfukie, Mama huyu alishindwa kuendelea kwa kuwa Watu waliona”

Kamanda Issah alisema sababu ya Mwanamke huyo kutekeleza mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kutokana na kupewa taarifa kuwa Mume wake aliyetengana nae kwa muda ako katika mapenzi na Mwanamke mwingine.