Eritrea yakusanya askari wa akiba kwa ajili ya vita vya Tigray

Baadhi ya askari wa akiba waliambiwa walete vifaa vyao wenyewe kama vile blanketi na chupa za maji.

Muhtasari

• Askari wa akiba katika maeneo mengine mengi ya nchi pia wameambiwa kuripoti katika ofisi zao kuu.

Shughuli ya kuwakusanya wanajeshi wa akiba inaendelea nchini Eritrea ambapo askari wa akiba hadi umri wa miaka 55 wameitwa kurejea jeshi tena, ripoti zinasema.

Siku ya Alhamisi, wengi katika mji mkuu, Asmara, walipewa notisi na kupelekwa mstari wa mbele wa vita saa chache kwenye mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na eneo la Tigray nchini Ethiopia, vyanzo viliiambia BBC Tigrinya.

Askari wa akiba katika maeneo mengine mengi ya nchi pia wameambiwa kuripoti katika ofisi zao kuu.

Hivi majuzi, shughuli za kuwasaka watu kurejea jeshini zimeimarishwa katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na Asmara. Vikosi vya usalama vinawazuia watu kuangalia kama wana msamaha wa kutohudumu katika jeshi .

Baadhi ya askari wa akiba waliambiwa walete vifaa vyao wenyewe kama vile blanketi na chupa za maji, vyanzo vinasema.

Kulikuwa na matukio ya kina mama, watoto na wake wakilia wakati wa kuwaaga wana, baba, kaka na waume zao.

Uhamasishaji wa hivi punde umezua hofu kwamba mzozo katika eneo jirani la Tigray nchini Ethiopia huenda ukaongezeka zaidi.

Mapigano kati ya serikali ya Ethiopia na vikosi vya Tigray yalianza tena mwezi uliopita baada ya kipindi cha mapigano kusitishwa.

Viongozi wa Tigray wameishutumu Eritrea kwa kuungana na kuwasiliana na Ethiopia katika maeneo ya magharibi ya mpaka wao wa pamoja.

Mamlaka zote za Ethiopia na Eritrea hazijajibu maombi ya maoni - lakini mamlaka ya Eritrea ilishutumu vikosi vya Tigray kwa kupanga kuwashambulia.

Vikosi vya Eritrea vilipigana pamoja na jeshi la serikali ya Ethiopia dhidi ya vikosi vya Tigrayakatika awamu ya kwanza ya vita. Walishutumiwa kwa ukatili - maafisa wa Eritrea walikanusha.

Marekani imeweka vikwazo kwa Wanajeshi wa Ulinzi wa Eritrea na chama tawala cha PFDJ kushiriki kwao katika mzozo wa Ethiopia.