Mwalimu afungwa miaka 30 jela kwa kumlawiti mwanafunzi wa darasa la sita

Mwalimu huyo alimuita mwanafunzi huyo kisha kumshrutisha avue nguo kabla ya kumtendea unyama huo

Muhtasari

• Mwalimu huyo Idrisa Athumani mweney miaka 29 alipunguziwa adhabu hiyo hadi miaka 30, siku mbili tu baada ya hukumu ya awali kumhukumu kifungo cha maisha.

Mwanaume aliyefungwa miaka 30 jela
Mwanaume aliyefungwa miaka 30 jela
Image: Mwananchi

Mahakama Moja nchini Tanzania katika mkoa wa Mara imempa adhabu ya miaka 30 jela mwalimu mmoja aliyepatikana na hatia ya kumlawiti mwanafunzi wake.

Mwalimu huyo Idrisa Athumani mweney miaka 29 alipunguziwa adhabu hiyo hadi miaka 30, siku mbili tu baada ya hukumu ya awali kumhukumu kifungo cha maisha.

Jarida la Mwananchi liliripoti kwamba Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Erick Marley alisema kuwa mahakama hiyo imejiridhisha pasi  na shaka kuwa mwalimu huyo aliyeajiriwa Desemba mwaka 2020 na kuanza kazi shuleni hapo Januari, 2021  alitenda kosa hilo kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.

"Mahakama hii inakutia hatiani kutokana  na kosa uliloshtakiwa nalo na ili iwe mfano kwako wewe na wengine wenye tabia kama yako ukizingatia kuwa umekabidhiwa watoto ili kuwatunza na hili suala ni kinyume na tamaduni zetu, halitakiwi wala kuruhusiwa nakuhukumu kwenda jela miaka 30" Jarida la Mwananchi lilinukuu maneno ya hakimu huyo.

Akisoma maelezo ya shtaka hilo, hakimu Marley amesema kuwa mwalimu huyo alishtakiwa Julai 20, 2022 kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wake wa  darasa la sita mwenye umri wa miaka 12.

"Tukio lilifanyika tarehe ambayo bado haujajulikana Mei mwaka huu majira ya saa nane mchana baada ya mshtakiwa kumuita mwanafunzi wake akiwa na nia ya kutenda kosa hili" Kiongozi wa mashtaka alisema.

Mwananchi waliripoti kwamba siku ya tukio mwalimu huyo alimuita mwanafunzi huyo kisha kumtaka avue nguo agizo ambalo mwanafunzi huyo aligoma kutekeleza kisha mwalimu kumshika kwa nguvu na kumvua nguo kisha kumuinamisha na kutenda kosa hilo.

Alipotakiwa kujitetea mwalimu huyo ambaye ni mwalimu wa nidhamu shuleni kwake aliiomba mahakama hiyo kumpa adhabu ndogo kwani yeye ni baba wa familia mwenye mke mmoja na watoto wawili hivyo familia yake inamtegemea.