Mwanaume amuuwa mkewe baada ya ramli ya mganga kumuonesha ni adui yake

Baada ya kupigiwa ramli na mganga, aliambiwa mbaya wake ataonekana ndotoni na kutakiwa kumuua

Muhtasari

• Alimuuwa mkewe na kuutupa mwili katika dimbwi la maji ili kutokomeza Ushahidi wa kitendo chake cha kinyama

Image: Instagram//Azam

Visa vya watu kuamini katika kupigiwa ramli na waganga katika nchi Jirani ya Tanzania si jambo geni.

Polisi katika mkoa wa Tabora nchini humo wanasemekana kumshikilia jamaa aliyemuua mkewe kwa kudai kwamba ni kufanya jinsi ramli ya mganga ilivyomuelekeza.

Mwanaume huyo aliyetambuliwa kwa jina Idd Mkonongo alimuuwa mkewe na kuutupa mwili katika dimbwi la maji ili kutokomeza Ushahidi wa kitendo chake cha kinyama.

Vyombo vya habari nchini humo viliripoti kwamba Mkonongo alienda kwa mganga na kupigiwa ramli ambapo aliambiwa baadae usiku angemuona mbaya wake kwenye ndoto.

Alipolala usiku ndoto ikamjia ikimuonesha kwamba mkewe ndiye adui wake aliyetambiwa na mganga na ndipo aliamka, akachukua kifaa butu na kumpiga mkewe hadi kufa kwa kuwa ndoto ya ramli ile ilimuonesha huyo ndiye adui yake mbaya asiyemtakia mazuri. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilisha taratibu za uchunguzi dhidi ya mauaji hayo.

Habari hizi zinakuja siu chache tu baada ya jamaa mwingine kufikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la kumroga mtoto wa ndugu yake.

Jamaa huyo alishtakiwa kwamba baada ya familia hiyo kuenda kwa mganga na kupigiwa ramli, ilionekana kwamba binamu mtoto ndiye mlozi na hivyo mahakama ikampa kibano cha miaka 5 jela.

Baada ya wiki moja, habari hizo zilisambaa na ikaripotiwa kwamba jamaa huyo aliachiliwa huru kwani vyombo vya dola siku zote havijihusishi na masuala ya ushirikina ambayo hayana Ushahidi.